Na Mwandishi wetu, Karatu Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, leo tarehe 16, 2025, amezindua Makumbusho ya kisasa ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai (Urithi Geo Museum) baada ya mradi huo kukabidhwa na Serikali ya China kwa Serikali ya Tanzania katika eneo la Karatu mkoani Arusha.
Mradi huo uliogharimu shilingi Bilioni 32 ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao ulilenga kuboresha miundombinu ya utalii, ujenzi wa makumbusho ya kisasa ya jiolojia na kuendeleza shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro-Lengai (Ngorongoro-Lengai Geopark Development Project)
Akifungua makumbusho hiyo Dkt. Mpango ameeleza kuwa Tanzania kupitia eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilipewa hadhi ya kuwa eneo lenye utalii wa Miamba “Geopark” mwaka 2018 na kuwa Geopark Pekee katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na ya Pili kwa Afrika na kusisitiza kuwa kukamilika kwa makumbusho hiyo kutavutia wageni kutembelea na kupata taarifa za Jiolojia.
Dkt. Mpango, amesisitiza kuwa uendeshaji wa mradi wa makushusho hiyo mpya uende sambamba nakutoa mafunzo kwa watumishi watakaohudumia wageni wanaotembelea makumbusho hiyo, kutunza na kuboresha miundombinu, kusaidia na kushirikisha Jamii inayozunguka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii ambavyo ni hazina ya nchi.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amesema mradi huo ambao ni wa aina yake barani Afrika chini ya mpango wa “Belt and Road Initiative”, unadhihirisha ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Tanzania ulioanza tangu mwaka 1964.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema eneo la Ngorongoro pamoja na kuwa na hadhi ya Jiopaki pia limeshinda tuzo ya kuwa kivutio cha utalii Barani Afrika mwaka 2023 na 2025 kupitia mtandao wa World Travel Awards.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Venance Mabeyo ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu ya hifadhi ya Ngorongoro na kusema makumbusho ya Urithi ni moja ya kazi kubwa ya serikali katika kuendeleza mazao mapya ya utalii.