*Tahadhari yatolewa katika matumizi ya miundombinu hiyo.
Na Mwandishi Wetu.
Kiu ya muda mrefu ya wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani ya kupata usafiri wa uhakika na wa kuaminika sasa imekatwa rasmi, baada ya kuanza kwa huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Mbagala Rangitatu hadi Gerezani Kariakoo.
Huduma hiyo imeanza rasmi Oktoba 12, 2025 baada ya kukamilika kwa mageti janja na mfumo wa kidijitali wa matumizi ya kadi, hatua iliyowezesha Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuruhusu abiria kuanza safari kwa urahisi na usalama zaidi.
Katika hali isiyo ya kawaida, wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani walionekana wakiwa na furaha isiyopimika huku wengine wakipiga picha kwenye mabasi hayo na kuposti katika mitandao ya kijamii wakionesha shukrani kwa Serikali kwa kuwaletea huduma hiyo.
Wananchi Wafurahia Hatua Hiyo
“Ndugu yangu, sisi wakazi wa Mbagala sasa tumekumbukwa. Mambo haya tulidhani hayawezekani, ila leo nashuhudia kwa macho yangu mabasi ya mwendokasi yakifanya kazi. Tunashukuru sana Serikali kwa maendeleo haya,” alisema Fikiri Almasi, mkazi wa Mbagala Charambe.
Naye Mwanahamisi Abdalah, mkazi wa Mtoni Mtongani, alisema ni muhimu wananchi kuzingatia ustaarabu wa matumizi ya miundombinu hiyo mpya ili huduma iwe endelevu.
“Ni vizuri tukaitunze miundombinu hii, tusiharibu mabasi wala mageti, maana tumeteseka kwa muda mrefu kupata usafiri wa uhakika,” alisema.
Foleni za Wananchi Kununua Kadi
Mwandishi wetu alipotembelea vituo vya kuuza kadi janja za mwendokasi ikiwemo Gerezani, Mtoni Mtongani, Kwa Aziz Ali, Zakhem na Rangitatu, alikuta foleni ndefu za wananchi waliokuwa wakinunua kadi hizo ili kuanza kutumia huduma.
Awali, DART ilifanya kampeni ya kuhamasisha wananchi kununua kadi hizo kwa kutumia magari maalumu ya matangazo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi – Kikosi cha Usalama Barabarani, lakini mwitikio ulikuwa mdogo kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uhakika wa kuanza kwa huduma.
Kwa sasa, DART imeeleza kuwa kila abiria anatakiwa kuwasilisha mojawapo ya vitambulisho vifuatavyo wakati wa kusajili kadi yake: Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya NIDA, Kitambulisho cha Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Pasipoti au Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.
Kanuni za Matumizi ya Huduma
DART imetoa mwongozo wa matumizi salama wa huduma hiyo, ikiwataka abiria:
-Kuwapisha wenye mahitaji maalumu kama wazee, wajawazito, wagonjwa na watu wenye ulemavu;
-Kuepuka kubadilishana mizigo kati ya abiria walioko ndani na nje ya kituo;
-Kutoingia na mizigo inayozidi kilo 20 au yenye hatari ya milipuko kama gesi, petroli au betri za magari;
-Kutupa taka kwenye vifaa maalumu vilivyowekwa ndani ya mabasi na vituoni;
-Kutoingia na mimea au wanyama hai ndani ya mabasi.
Aidha, wananchi wamekumbushwa kuepuka kufanya biashara kwenye miundombinu ya mwendokasi, madaraja ya waenda kwa miguu na maeneo ya maegesho.
Pia, magari binafsi, pikipiki, bajaji, baiskeli na guta yamepigwa marufuku kutumia barabara za mwendokasi.
Awamu za Mradi wa BRT
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam unatekelezwa kwa awamu sita.
Awamu ya Kwanza ni Kimara – Kivukoni/Gerezani/Morocco/Muhimbili, wakati Awamu ya Pili, iliyokamilika sasa, ni Mbagala – Gerezani – Kivukoni.
Awamu ya Tatu ipo katika Barabara ya Nyerere hadi Gongolamboto, Awamu ya Nne ni Katikati ya jiji hadi Mwenge – Tegeta, Awamu ya Tano inahusisha Barabara ya Mandela – Kigamboni, na Awamu ya Sita itahusisha Kimara – Kibaha na Mbagala – Vikindu.
Huduma hiyo imepokelewa kama hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa usafiri wa umma, kupunguza msongamano wa magari, na kuinua ubora wa maisha kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.