Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Oktoba 16, 2025
Jeshi la Polisi mkoani Pwani linachunguza tukio la kutatanisha baada ya miili ya watu wanne wasiojulikana kupatikana pembezoni mwa barabara ya kutoka Mapinga kuelekea Kibaha, katika maeneo ya Kidimu-Vingunguti, wilayani Kibaha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, miili hiyo iligunduliwa kufuatia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidimu, ambaye aliarifu vyombo vya dola kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 16, 2025 Morcase alifafanua baada ya taarifa kupokelewa, kikosi cha askari polisi kikiambatana na wataalamu wa uchunguzi wa makosa makubwa kilifika eneo la tukio na kukuta miili ya wanaume wanne waliokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 19 hadi 22.
“Watu hao hawakuwa na vielelezo vya utambulisho, na walikutwa na majeraha usoni na kwenye miguu,” alieleza Kamanda Morcase.
Miili hiyo ilihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi wa kidaktari, ambapo baadaye baadhi ya ndugu na wazazi waliweza kuitambua.
Kamanda Morcase alitaja waliotambuliwa kuwa ni Mikidad Abbas Mikidad (21), Hassan Juma Jumanne (21), wote wakazi wa Tabata Chang’ombe na maday worker wa bodaboda; Fadhil Patrick Hiyola (19), mkazi wa Vingunguti Miembeni, pia mwendesha bodaboda; na Abdallah Fadhil Nyanga (21), dereva wa bajaji mkazi wa Kisukuru Tabata.
Baada ya uchunguzi wa awali kukamilika, miili ya marehemu hao imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo na wahusika wa mauaji hayo, na limewataka wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi huo kujitokeza na kuwasiliana na vyombo vya dola.
“Tunaomba ushirikiano wa wananchi, Taarifa yoyote muhimu itapokelewa na kuchukuliwa hatua za haraka,” aliongeza Kamanda Morcase.