Na Mwandishi wetu, Arumeru
NAIBU Waziri wa Madini Dkt Stephen Kiruswa, wagombea ubunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassary, wa Simanjiro James Ole Millya na aliyekuwa mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka, wamewaongoza mamia ya wakazi wa mikoa ya Arusha na Manyara, kwenye mazishi ya mama wa mmoja wa wamiliki wa kitalu C katika machimbo ya madini ya Tanzanite Onesmo Mbise yaliyofanyika kijiji cha Kwaugoro Wilayani Arumeru.
Mama wa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite ya Franone Mining LTD inayomiliki kitalu C, Onesmo Mbise, marehemu Apaililia Metasheiye Mungure amezaliwa mwaka 1954 na kufariki dunia mwaka 2025 na kuzikwa katika kijiji cha Kwaugoro wilayani Arumeru.
Naibu Waziri Dkt Kiruswa, akizungumza kwenye maziko hayo ametoa pole kwa wakazi wa eneo hilo na kuwaombea faraja kwa Mungu kwenye kipindi hiki kigumu cha msiba.
Amesema wafanyakazi wa Wizara ya Madini sekta ya madini kwa ujumla wanatoa pole kwa Onesmo Mbise kwa msiba mkubwa wa kufiwa na mama yake mzazi.
“Pia Waziri wangu wa Madini mheshimiwa Anthony Mavunde ametuma salamu za rambirambi kwani hakuweza kufika kutokana na majukumu ya kampeni kanda ya ziwa,” amesema Dkt Kiruswa.
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Manyara, Warda Albeid Maulid ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro amewasilisha salamu za rambirambi katika msiba huo.
“Nipo hapa kwa niaba ya RC wetu mheshimiwa Queen Cuthbert Sendiga na DC wetu mwalimu Fakii Raphael Lulandala ambao wamepata udhuru na kuniagiza niwakilishe Serikali ya Manyara katika msiba huu,” amesema Warda.
Mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassary ametoa pole na kuwashukuru wageni wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika msiba huo.
Nassary ameeleza kwamba kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo wanatoa shukrani za dhati kwa kumsindikiza mama yao mpendwa Apaililia Mungure katika nyumba yake ya milele.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya ameeleza kwamba japokuwa hajawahi kuonana na mama huyo ila mtoto wake Onesmo Mbise amekuwa msaada mkubwa kwa jamii.
Ole Millya amesema wanashukuru Mungu kwa maisha ya mama Apaililia Mungure hapa duniani na kumzaa Onesmo Mbise ambaye amekuwa faraja kwa watu wengi.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi ametoa pole kwa familia hiyo na akieleza kuwa watu wengi wamejitokeza kwa wingi kumpa pole Onesmo Mbise kwani ni mtu anayejitoa kwa jamii.
“Umati mkubwa wa watu umefika kutoa pole kwa familia kutokana na namna mtoto wa boma hilo Onesmo Mbise anavyoishi vyema na jamii anayofanya nayo kazi,” amesema Elisha.
Mwenyekiti wa chama cha mabroka Tanzania (CHAMMATA) Jeremiah Simon Kituyo ametoa pole kwa Onesmo Mbise na familia kwa ujumla kutokana na msiba huo.
“Mbise ni mtu anayeishi na watu vyema na pia kupitia kampuni ya Franone wamekuwa wazaliwa wa kwanza kutoa madini yao kwenye gulio la kwanza tuliloliandaa,” amesema Kituyo.
Mbunge mstaafu wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka ametoa pole na kuipongeza familia hiyo kwa namna wanavyoishi maisha yao bila kubaguana.
“Hapa huwezi kujua yupi mtoto wa baba mkubwa, baba mdogo, mama mkubwa, mama mdogo au mtoto wa mjomba wala shangazi ni upendo tuu uliotawala kwa ndugu wote,” amesema Sendeka.
Mkazi wa kijiji cha Kwaugoro Kisali Nginana amesema kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake ameona watu wakibeba chakula kwenye msiba kwani kilikuwa kingi.
“Msiba ulikuwa mkubwa watu wamekula hadi wakasaza wamebeba nyama, wamebeba shaba, kweli hii ilikuwa sherehe ya mwisho ya maisha ya bibi yetu Apaililia Mungure ambaye ameagwa kwa heshima kubwa,” amesema Nginana.