Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno, amesema serikali imejipanga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zake za kisheria ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mhe. Maneno alitoa kauli hiyo leo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha taasisi za kisheria kinachofanyika mjini Kibaha, mkoani Pwani, ambacho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Amesema kikao hicho ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi na kufuata misingi ya sheria, uwajibikaji na weledi, kwa lengo la kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/2030.
“Tunataka kuhakikisha kila shirika la umma linafanya kazi kwa ufanisi, kwa kufuata misingi ya sheria na weledi, ili mchango wao uweze kuonekana katika maendeleo ya taifa,” amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema Serikali inataka mashirika ya umma kujiwekea mikakati madhubuti itakayowezesha kuongeza mapato, kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Posi, amesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuongeza ufanisi na ushindani katika soko la kimataifa.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kinatarajiwa kujadili changamoto zinazozikabili taasisi hizo, kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji, pamoja na kuimarisha mahusiano baina yao kwa manufaa mapana ya taifa.
Washiriki wanatarajiwa pia kuibua mapendekezo ya kisera yatakayosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mali za umma, kuendeleza uwazi na uwajibikaji, sambamba na kuimarisha mchango wa taasisi za kisheria katika kukuza uchumi wa taifa kwa mujibu wa dira ya Serikali.