Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Beate MeinI-Reisinger.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) unaofanyika Kampala, Uganda kuanzia tarehe 13 hadi 16 Oktoba 2025.
Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Austria ikiwemo masuala ya Elimu, Afya, Utalii, Biashara, Uwekezaji na Mafunzo.
Mhe. Chumi ameiomba Serikali ya Austria kuwashawishi raia wao kuja kuwekeza nchini, kufanya biashara na kutalii. Vilevile, ameiomba Austria kuongeza idadi ya nafasi za maafisa wa Serikali wanaenda kujifunza nchini humo.
Kwa upande wake, Mhe. MeinI-Reisinger ameishukuru Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo na Austria na kupongeza amani iliyopo nchini na kusema kuwa amani hiyo ndio kichocheo kikubwa kwa kampuni kubwa za Austria, watu binafsi kuja kuwekeza nchini pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu.
Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini Austria mwaka 2022 na Austria inawakilishwa nchini kupitia Ubalozi wake uliopo jijini Nairobi.