Serikali imeipatia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) magari mapya 140 ili kuboresha zaidi utendaji kazi wa Mamlaka hiyo, hatua ambayo imepokelewa kwa mikono miwili na hasa ikizingatiwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zlizokuwa zikiikabili Mamlaka hiyo ilikuwa ni uhaba mkubwa wa magari.
Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma zake katika nyanja mbalimbali ikiwemo usajili na utambuzi wa watu nchini unaotekelezwa na NIDA, na inaonyesha dhamira ya dhati ya serikali ya kusogeza huduma zake kwa wananchi.
Aidha, hatua hii ya serikali kuipatia NIDA magari hayo inalenga pia kusaidia kuimarisha utekelezaji wa maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu Jamii Namba kwa kuanza kusajili wa watoto kuanzia wanapozaliwa na kupewa utambulisho wa Taifa unaojulikana kama Jamii Namba ili kuwawezesha kupata huduma za Kijamii na Kiuchumi zinazohitaji Utambulisho wa Taifa badala ya kusubiri wafikishe miaka 18.
Magari haya yatasaidia pia kukabiliana na changamoto ya kuwafikia wananchi wakati wa kutoa huduma za usajili na utambuzi wa watu katika baadhi ya vijiji viliyo mbali na makao makuu ya wilaya zilipo ofisi za NIDA.
Akikabidhi baadhi ya magari hayo kwa Maafisa usajili wa Wilaya za Uvinza, Sumbawanga, Mpanda na Karagwe jana katika ofisi za Makao Makuu ya NIDA jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA James Kaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia NIDA magari hayo. Ametaka magari hayo yatumike kama ilivyokusudiwa ili kuleta tija kwa Mamlaka na Taifa kwa ujumla.
“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutapatia magari haya ambayo tunaamini ni miongoni mwa vitendea kazi muhimu utekelezaji wa majukumu yetu” amesema Kaji.
Amesema serikali imetumia fedha nyingi kununua magari hayo hivyo ni vema yakatunzwa na kutumika vizuri sambasamba na watumishi wote wa NIDA kuchapa kazi kwa bidii na kwamba kila ofisi ya NIDA ya wilaya itapatapatiwa gari.
Mpaka sasa tayari Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa imepokea magari kumi na saba (17) ambayo yamesambazwa katika ofisi za NIDA katika wilaya mbalimbali nchini kwa lengo la kufikisha huduma kwa wananchi kwa haraka. Magari mengine yataendelea kuwasili katika awamu mbalimbali mpaka yatakapo kamilika.