Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimehimiza matumizi ya matokeo ya tafiti katika kuchangia sera na mipango ya maendeleo ya taifa, kikiweka msisitizo kwenye utekelezaji wa miradi mipya 36 ya tafiti yenye thamani ya shilingi bilioni 10.5.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Bw. Andrew Massawe, aliyasema hayo katika mahafali ya 46 ya SUA yaliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro.
Amesema kati ya miradi hiyo, miradi 10 inafadhiliwa na wadau wa kimataifa, miradi 2 inafadhiliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), huku miradi 24 ikifadhiliwa na chuo kupitia mapato yake ya ndani.
Bw. Massawe alieleza kuwa tafiti zinazofanywa SUA zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza maarifa na kutatua changamoto katika sekta za kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii, hivyo kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.
Aidha, alibainisha kuwa Baraza linafuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo 2021–2026, sambamba na malengo tisa ya kimkakati, ili kuongeza tija na ufanisi. Hadi sasa, utekelezaji wa mpango huo umefikia asilimia 85.
Masawe aliwataka wahitimu kuzingatia kuwa ulimwengu wa kazi na maisha ya kijamii hubadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya mazingira, hivyo ni muhimu kubadilika kulingana na wakati, kutumia maarifa waliyojipatia kujiajiri na kuwaajiri wengine.
Baraza la Chuo Kikuu cha SUA limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa kitovu cha ubora katika elimu ya juu, utafiti, na utoaji wa huduma kwa jamii.
Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, Baraza limefanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kuboresha ufanisi wa chuo, ikiwemo kusimamia mapato na matumizi kwa uwazi, uwajibikaji na nidhamu ya kifedha. Pia limeimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani, kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha SUA inakidhi vigezo vya ukaguzi wa ndani.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Msafara wa Wanataaluma (MLAU), Prof. Kalunde Sibuga alisema kuwa akiwa mbebaji wa alama za kitaaluma za wahitimu, ikiwemo siwa au rungu linaloashiria mamlaka ya kitaaluma na kitabu kinachoashiria safari ya maarifa, aliongoza maandamano ya wahitimu waliokuwa wakionekana wakiwa na furaha na fahari kubwa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, alisema kuwa jumla ya programu 85 zilihusisha wahitimu 3,560, wakiwemo wanaume 2,029 na wanawake 1,531. Kati yao, 3,275 walihitimu shahada za kwanza, 127 shahada za umahiri, 18 shahada za uzamivu (PhD), 100 stashahada na 38 astashahada.