Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SIMU iliyopigwa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuniita Ikulu binafsi imenishutua sana, na zipo sababu kadhaa zilizofanya niogope.
Kuitwa Ikulu na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan tena katika wakati huu wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu ilinifanya niwe na hofu,wasiwasi ulitanda moyoni.Kulikoni naitwa na Rais Samia Ikulu?
Nakumbuka ilikuwa ni Oktoba 10 mwaka huu, ilipopigiwa simu ngeni kupitia namba yangu ya 0713833822, kwanza ilipopigwa mara ya kwanza sikupokea na sikupokea kwasababu ilikuwa ngeni, baada ya kupita dakika tano ikapiga tena namba ile ile, nikasema ngoja niipokee.
Nikachukua simu yangu ya kitochi na kubonyeza kile kitufe cha kupokelea simu, ile napokea tu nikasikia sauti ikinisalimia kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nikajibu kazi iendelee lakini nikawa najaribu kuisikiliza sauti.

Kwa bahati nzuri wakati natafakari nani anapiga, akajitambulisha kwamba “naitwa Rais Samia Suluhu Hassan na kwasasa ni Mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu” alivyojitambulisha tu nikaona mwili kama umekufa ganzi, nilikuwa nimesimama nakatafuta tofali nikakaa ili nisikilize anataka kuniambia nini.
Nilichokifanya nikamsalimia kwa kumpa heshima yake, Shikamoo mama na Rais wangu mpendwa. Akaitikia na kisha kuzungumza maneno mafupi tu , “nakuhitaji uje Ikulu nina mazungumzo na wewe Saidi Mwishehe”
Naitwa na Rais wakati huu wa kampeni? Kuna nini nimefanya kwake au kwa nchi yangu? Hakika nilijikuta moyo unaenda mbio, mapigo ya moyo yakaongezeka kama vile nimekimbizwa na wasiojulikana.
Lakini nikajipa moyo na kumjibu Rais Samia nimepokea maelekezo yako. Nikamuliza, nije lini maana najua uko katika ratiba za mikutano yako ya kampeni kuelekea Oktoba 29 ambapo Watanzania watatimiza takwa la Kikatiba kuchagua Rais,Wabunge na Madiwani. Akasema uje kesho Ikulu ya Chamwino,Dodoma.
Nakumbuka alipiga simu saa tano asubuhi na baada ya simu yake kukata nikaanza kutafakari kuna nini ambacho Dk.Samia ananiitia Ikulu? Mbona sina cheo, sina ukubwa, sio maarufu, sio mkosefu, sina tabia za hovyo.Yaani anaiita Ikulu tena wakati huu ambao Watanzania wanasubiria kutiki Oktoba 29.
Yaani najiuliza hivi Rais wetu Dk.Samia ambaye kwa sasa anaomba tena ridhaa ya wananchi ili arejee katika usukani wa kuongoza nchi yetu namba yangu ya simu amepewa na nani? Mbona sina anayenijua, mbona sina urafiki na mkubwa yeyote? Hivi Dk.Samia ananiitia nini mimi, mtu niliye kapuku na sina mbele wala nyuma.
Niliwaza mambo mengi sana, nikaanza kujifanyia uchunguzi binafsi ili nitafute kama kuna kosa nimelifanya katika nchi yangu, nikakuta sina, nikajaribu kuwaza labda nimemkosea lakini najikuta sijamkosea Rais wangu, kwanza nampenda, namheshimu na hakika sina shaka naye hata kidogo.
Nikasema wala isiwe tabu, kesho nitakwenda kama alivyotaka. Nikasema nitakwenda kumsikiliza na niko tayari kwa kumsikiliza na kupokea maoni na ushauri wake. Lakini usiku niliamua kutenga muda wa kumuomba Mungu safari yangu ya kwenda kuonana na Mgombea Urais wa CCM Dk.Samia ikawe yenye heri.

Jua lilipochomoza kama kawaida ya binadamu wengine wote ratiba ya asubuhi ikachukua nafasi yake lakini muda wote nawaza leo ndio siku ya kukutana na Rais Samia.
Siku hiyo niliondoka nyumbani mapema ili nisichelewe Ikulu kama ambavyo Mgombea Urais Dk.Samia alivyoniambia katika simu yake ya kuniita Ikulu ya Chamwino,Dodoma.
Nakumbuka saa mbili asubuhi nikawa nimefika pale Ikulu Chamwino tayari kwa kumuona mgombea Urais na Rais wetu Dk.Samia. Kama unavyojua upendo wa Rais kwa watu wake kwa kweli alinipokea kwa upendo mkubwa sana, hata ile hofu yangu ya kuonana naye ikawa imepungua ingawa Rais hazoeleki.
Yaani kuna wakati naona kama mapigo yangu ya moyo yanapoteza muelekeo wake katika kusukuma damu. Nahisi Mama Samia aligundua nina hofu hivyo alinitania vipi mwanangu Mwishehe, unaendeleaje? Nikamjibu naendelea vizuri kisha nikawa kimya. Kukutana na Rais wee bwana weee lazima utapagawa tu.
Tangu aliponipokea pale Ikulu ya Chamwino muda wote akili yangu nikawa najiuliza tu hivi kuna jambo gani, Dk.Samia Rais anataka kuniambia nini? Huu ni wakati wa uchaguzi kuna nini nimefanya? Sikuwa na jibu lakini nilijipa moyo ngoja nione nimeitiwa nini?
Hata hivyo kadri muda ulivyozidi kwenda ndio nilikuwa naona kabisa presha inapanda,presha inashuka. Ilikuwa siku ngumu kwangu. Oktoba 10 ,2025 itabakia katika kumbukumbu za maisha yangu yote. Kuitwa na Rais kusikie hivyo tu ,tena ukiwa hujui umeitiwa nini.
Nakumbuka vizuri sana,kwenye mazungumzo yetu na Mama Samia tulikuwa wawili tu, aliwaondoa wasaidizi wake ,hakutaka wasikie tunachozungumza. Wakati wasaidizi wake wanaondoka nikajiuliza Inawezekanaje tubaki wawili ?
Kuna nini? Hili ndio swali ambalo nilikuwa najiuliza kichwani lakini sikutaka kuonesha woga wangu mbele yake. Muda wote nilikuwa natabasamu usoni lakini huko ndani utumbo ,figo na maini nilihisi vinagongana. Hata hivyo kwa jinsi alivyo Dk.Samia nilikuwa najua niko salama.
Ni mama mwenye huruma, mama mwenye upendo, mama mwenye busara na hekima kubwa kwetu. Mungu amemjaliaa utulivu mkubwa na nilipokuwa nawaza hayo yote nikawa najisemea mwenye mazungumzo yetu yatakuwa na nia njema.
Ngoja nieleze ilivyokuwa baada ya kuwaondoa wasaidizi wake wote akaniambia mwanangu Mwishehe nimekuita nina mazungumzo na wewe.Akaendelea kuniambia najua unajiuliza kwanini nimekuita wewe na ni wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Kwa kweli sikuwa na la kumwambia, nilisema tu Mheshimiwa Rais wangu na Mgombea Urais kupitia CCM nimekuja,nimeitikia mwito wako na niko tayari kupokea maoni,ushauri na maelekezo yako. Nitayatii na kuyaheshimu yote utakayoniambia.Niko tayari Mama.
Baada ya kusema hivyo akaniambia ameniita kwasababu kuna mambo anataka kufahamu kutoka kwangu kwa niaba ya wananchi walio wengi hasa kule chini kabisa.
Akaniambia anao wasaidizi na washauri wake lakini kabla ya Oktoba 29 anataka kusikia maoni ya Watanzania wengine, “Na Mwishehe nimeona ni mtu sahihi”. Nikajibu kwa kifupi tu Mama Ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mgombea Urais Dk.Samia baada ya kutoa maelezo hayo akaniambia anataka tuzungumze kuhusu mwenendo wa kampeni zake za kuomba kura kuelekea Oktoba 29 mwaka huu.
Majibu yangu kwa mgombea Urais Dk.Samia ni kwamba mwenendo wa kampeni ni mzuri, tangu uliopozindua kampeni Agosti 28 mwaka huu pale Kawe mkoani Dar es Salaam hadi sasa umefanya kampeni ambazo zimejikita katika kuelezea yale ambayo Serikali unayoiongoza imeyafanya katika miaka mitano iliyopita na yale ambayo unatarajia kuyafanya miaka mitano ijayo iwapo Watanzania watakupa ridhaa ya kuongoza nchi.
Lakini pia nikwambie mwenendo wa kampeni zako umejikita katika kuinadi Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 ambayo kimsingi imelenga kuboresha maisha ya watu katika nyanja mbalimbali.Lakini kauli mbiu ya Kazi na Utu imekuwa alama muhimu ambayo inakutambulisha.
Sio vizuri kumtania lakini nilimwambia Mama wewe Mungu amekujaalia utu na nadhani ndio maana CCM ikaona bora kwenye Ilani yake iweke Kazi na Utu .Najua katika nchi kubwa kama hii sio wote wana moyo wa aina yako. Moyo wenye utu. Hongera Mama Samia ,Hongera Rais Samia,hongera mgombea Urais kwa kutuonesha Utu katika uongozi wako.
Wakati naendelea kuzungumzia mwenendo wa kampeni zake akaniuliza tena, “Ninayoyazungumza kuhusu Serikali katika miaka mitano ijayo mnayaelewa huko mtaani?”. Yaani swali hilo wala sikutaka kuchelewa nikajibu tena kwa kujiamini sana kwamba mtaani haya ambayo unayozungumza katika mikutano yako tunayaelewa sana.
Nakumbuka nilikwambia Mama haya ambayo unayazungumza yanagusa maisha yetu, yanagusa maendeleo yetu,yanagusa hatma ya Taifa hili. Nikatoa mfano moja ya jambo ambalo mtaani tume lipenda ni kupiga marufuku maiti kutozwa fedha katika hospitali zetu.
Ilikuwa kero kwa ndugu wa marehemu na ilikuwa inatengeneza chuki lakini Mama yetu, mama mwenye upendo unaenda kuindoa kero hiyo ambayo imekuwa ya muda mrefu na watangulizi wako walishindwa kuitafutia ufumbuzi. Ahsante Rais na Mgombea Urais.
Pia akaniuliza “Vipi kuhusu ahadi za bima ya afya ambayo katika siku 100 za mwanzo baada ya kuingia madarakani tunakwenda kuanza kwa majaribio kwa baadhi ya makundi ya wananchi hasa wasiojiweza” .
Nikamjibu ahadi hiyo mtaani imepokelewa kwa furaha kubwa, moja ya changamoto kubwa kwa Watanzania wengi ni katika kumudu gharama za matibabu hasa kwa magonjwa kama figo,moyo,mishipa ya ufahamu na sukari.Nikamwambia uamuzi wako kwamba Serikali itabeba gharama za matibabu umegusa maisha yetu moja kwa moja. Nikaendelea kumueleza katika gharama za matibabu hapa baadhi ya familia zimebakia kuwa masikini kwasababu fedha zimetumika kutibu mwanafamilia. Tunakushukuru mama kwa uamuzi huu wa kubeba gharama za matibabu.
Nikuahidi ule mpango wa Bima ya afya kwa wote Watanzania tunausubiria kwa hamu, tutajiunga kwa utaratibu ambao Serikali yako itauweka. Tuko tayari kuiunga mkono Serikali kwa kujiunga na bima ya afya kwa wote.
Katika mazungumzo yetu niliona kabisa anataka kunisikiliza mimi zaidi, maana alikuwa ananiuliza maswali mafupi kisha ananiacha nijibu.
Mgombea Urais Dk.Samia aliniuliza kuhusu wakulima wanasemaje? Nikamwambia Mama wakulima wa nchi hii wanakushukuru sana kwa jinsi ulivyobadilisha maisha yao, mfumo wa ruzuku za pembejeo ikiwemo mbolea ya ruzuku imesababisha wakulima kufurahia.
Wanapata mazao mengi ,wanavuna na kisha wanauza na kupata fedha nyingi.Umekifanya kilimo kuwa biashara inayolipa,kilimo chini ya uongozi wako sio mateso tena bali kimekuwa kimbilio la wengi, Watanzania tunajua thamani ya kilimo.
Ahsante sana Mama na ahadi yako ya kuendelea kutoa ruzuku tumeipokea kwa mikono miwili. Ahadi ya uwepo wa matrekta ambayo tutakodishiwa kwa nusu bei tunaisubiria kwa hamu.Wenye matrekta wametuumiza kwa muda mrefu na hatukuwa na kimbilio. Lakini Mama umeona hilo na umekuja na majibu yake.
Mama Samia akaniuliza tena vipi kuhusu wavuvi hapa nami nikajibu kwa kifupi tu kwamba mkakati wa Serikali kuendeleza wavuvi wa nchi hii wavuvi wenyewe ni mashahidi. Ukopeshaji vizimba kwa ajili ya kufuga samaki umekuja kubadilisha maisha yao.
Hapa nikwambia Mama Samia kuwa hongera kwa Serikali kuja na ile programu ya BBT ambayo yenyewe imejikita katika kujenga kesho iliyobora ambayo hii iko zaidi katika sekta ya kilimo,ufugaji na kwenye uvuvi.
Pamoja na hayo Mgombea aliuliza kuhusu ahadi zake katika kutatua changamoto ya maji nchini. Hapa nako nikamjibu kwa kujiamini kuwa mkakati wa kuwa na gridi ya maji ya taifa hiyo inakuja kumaliza kabisa changamoto ya maji.
Lakini nikawambia mradi wa kutoa maji ziwa Victoria ambao Serikali yako imeendelea kuutekeleza umeondoa changamoto ya uhaba wa maji katika mikoa mingi ikiwemo ya Kanda ya Ziwa lakini hata Tabora ,Singida na mradi huo utakwenda mpaka Dodoma.
Mkakati wa kutua ndoo mama kichwani nao umesaidia kumfanya mwanamke wa Tanzania kuondokana na adha ya kufuata maji umbali mrefu.Na hapa nikamshukuru kwa hatua ambazo amezichukua katika maji.
Kwa kweli tulizungumza mengi. Hata swali la Rais Samia kuhusu amani ya nchi yetu nako nilimjibu kwamba Watanzania tunakushukuru kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa na amani, umoja na mshikamano.Tunajua unafanya kazi kubwa kuhakikisha Taifa letu liko salama. Vyombo vya ulinzi na usalama chini ya uongozi wako viko salama.
Aliponiuliza kuhusu miundombinu ya usafiri na usafirishaji nako nilimjibu mgombea Urais kuwa kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu imeelezwa vizuri na Maelezo yako kuhusu miundombinu ya barabara, reli hasa ya SGR ,meli na ndege tumekuelewa vizuri.
Hapo sitaki kutia neno lakini kwa kifupi mtaani tumekuelewa vizuri. Reli ya SGR kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma inathibitisha unayoahidi katika Ujenzi wa reli ya SGR yanakwenda kutekelezeka.
Pamoja na hayo Mgombea Urais akaniuliza kwa ujumla mtaani wanasemaje kuhusu Serikali katika miaka mitano iliyopita. Nilimjibu kwamba tunaipongeza Serikali kwa yote ambayo imeyafanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Nikamwambia chini ya uongozi wako kila kundi katika jamii yetu limeguswa na maendeleo yako. Kwa kifupi Mama umeupiga mwingi. Hongera.
Hata hivyo Dk.Samia akaniambia vipi kuhusu Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 Watanzania mmeshamua kura yenu inakwenda kwa nani? Swali hili lilinifanya nijione Kama Christiano Ronaldo au Lionel Mess wanapokuwa uwanjani.
Unajua kwanini ni swali ambalo kwangu niliona majibu yake yanaeleweka kwa haraka zaidi. Nilimjibu tena kwa tabasamu sana kwamba OKTOBA 29 tunakwenda Kutiki kwa Samia .Tumaini la Watanzania liko kwako,Uongozi wako katika miaka minne na nusu umetuthibitishia kiongozi sahihi anayeweza kutuvusha kwasasa ni wewe Dk.Samia Suluhu Hassan mama wa Kazi na Utu.
Baada ya kumjibu kuwa Watanzania tumeshaamua kura zetu zote ni za kwake ifikapo Oktoba 29 akaniuliza tena “Mtaenda kupiga kura?” hapa nikamjibu Mama katika uchuguzi mkuu mwaka huu Watanzania wana jambo lao.Wanataka kukupa kura za heshima.
Tumekubaliana tutajitokeza kwa wingi tena mapema asubuhi. Tunataka tuwaambie wenye husda na chuki Watanzania tuko na Samia kwenye shida na raha na kupitia Uchaguzi Mkuu mwaka huu tunataka kuthibitisha kwa vitendo kupitia sanduka la kura. Majibu yangu haya nikamuona Mama Samia anatabasamu na kucheka.
Hata hivyo nilishangaa kuona Mama Samia amenyanyuka na kuja nilipokuwa nimekaa pale Ikulu ya Chamwino, alivyosimama nami nikasimama akanipa mkono wake kama ishara ya kufurahia mazungumzo yetu.
Akaniuliza swali ambalo sikutarajia kama angeniuliza. Ni swali gumu ambalo kwa kweli limenitoa jasho usoni na wakati nataka kujibu nikawa kama nimeshituka hivi. Najiangalia vizuri kumbe nilikuwa ndotoni. Sikuwa na mazungumzo yoyote na Rais, wala hajanipigia simu ya kuniita Ikulu.
Usingizi wa mchana bwana na hivi nilishiba ugali na maharage mwenyewe nikawa najiona nimepata bahati Kuitwa na mgombea Urais Dk.Samia kumbe ni ndoto tu. Narudia tena jamani hii ni ndoto na anaweza kuota yeyote na wakati wowote.
Mgombea Urais Dk.Samia najua mimi nimeota ndogo hii ya mchana, lakini naamini ni ndoto njema na ujumbe wangu kwa Watanzania Oktoba 29 tukampigie kura. Mnisaidie ndoto yangu iwe kweli kwa kumpigia kura nyingi Samia Suluhu Hassan.
Halafu watu wengine sijui wakoje? nimesema kabisa hii ilikuwa ni ndoto sasa nikuulize na wewe nawe unachukua nini? Kwani nimekulazimisha usome nilichoandika. Acha ushamba bwana!! Kama umekasirika kunywa Sumu ili urest in piece.
Tuwasiliane mtu wangu