NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Chuo Kikuu Mzumbe kimepokea vitabu 69 vya kufundishia na kujifunzia kutoka Association of Chartered Certified Accountants (ACCA) kupitia ofisi yake ya Tanzania.
Vitabu hivyo vinahusu masomo ya uhasibu na fedha, na vinatarajiwa kusaidia walimu na wanafunzi katika kukuza maarifa ya kitaaluma na kiutendaji, hususan katika maeneo yanayohusiana na ushughulikiaji wa biashara, fedha, na mahitaji ya soko la ajira la kisasa.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Oktoba 17, 2025, katika Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe, ameishukuru ACCA kwa msaada huo, akisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha elimu ya uhasibu na fedha.
“Huu ni msaada mkubwa sana na utasaidia katika kuendeleza maarifa ya masomo ya uhasibu na fedha kwa walimu na wanafunzi wetu,” amesema Prof. Swalehe.
Kwa upande wake, Bw. Jenard Lazaro, Meneja wa ACCA Tanzania, amesema ACCA imekuwa mshirika wa muda mrefu wa Chuo Kikuu Mzumbe katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa uwezo wa walimu na usaidizi wa kitaaluma kwa wanafunzi.
“Tukio la leo ni mwendelezo wa ushirikiano wetu, na lengo kuu ni kuhakikisha wanafunzi wanapata vifaa bora vya kujifunzia vitakavyowawezesha kufanikiwa katika safari yao ya ACCA na taaluma zao za baadaye,” amesema Bw. Lazaro.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na wawakilishi wa chuo, akiwemo Dkt. Daudi Pascal Ndaki, aliyemwakilisha Mkuu wa Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, pamoja , Dkt. Joshua Mwakujonga, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Biashara, Ndaki ya Dar es Salaam pamoja na Bw. Elias Ntobi, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Maktaba Ndaki ya Dar es Salaam.
Uchangiaji huo unaakisi dhamira ya ACCA ya kuwezesha wataalamu wa fedha wa kizazi kijacho, kupitia kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu na taaluma, sambamba na kuinua ubora wa elimu ya uhasibu nchini Tanzania.