NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, amesema endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, moja ya mambo atakayoyapa kipaumbele ni kushughulikia ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Mkwawa, ambako kwa muda mrefu hakujawahi kuwa na kituo hicho.
Ngajilo amesema ukosefu wa kituo cha Polisi katika eneo hilo ni hatari kwa usalama wa watu na mali zao, hasa ikizingatiwa kuwa kata hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la watu kutokana na uwepo wa vyuo vya elimu ya juu na shughuli nyingi za wafanyabiashara.
Akizungumza katika mkutano wa kuomba kura uliofanyika kata ya Mkwawa, Ngajilo amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na usalama wa kudumu ikiwezekana wafanye shughuli za biashara hata nyakati za usiku.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa kituo hicho cha Polisi utakuwa miongoni mwa miradi ya kipaumbele atakayoshirikiana na Serikali kuitekeleza mara baada ya kuchaguliwa, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usalama kwa urahisi na uharaka zaidi.
“Kata ya Mkwawa ni eneo linalokua kwa kasi, lina vyuo, wafanyabiashara na wananchi wengi. Hatuwezi kuacha eneo kubwa kama hili bila kituo cha Polisi, ni wajibu wetu kuhakikisha usalama wa watu na mali zao unalindwa,” amesema Ngajilo
Alisema kuwa Kata ya Mkwawa imebeba jina la mtu mkubwa sana katika historia ya Tanzania aliyepambana na Wajerumani ili kuwalinda wananchi wake wa mkoa wa Iringa hivyo muhimu kuwa usalama kwa wananchi wa kata hiyo.
Aidha alisema kuwa kata hiyo imebeba heshima ndani na nje ya nchi yetu kwani Chifu Mkwawa Aliwaunganisha sana watu kuwa wamoja hivyo kata hiyo lazima iendelee kutokana na jina hilo.
Mambo yanayofanyika kata ya Mkwawa lazima iendane na maendeleo ya kata kwa jina sifa hivyo suala la Barabara ilani inasema endapo atachaguliwa atahakikisha barabara inayoanzia M.r. hotel Mpaka Pawaga inawekwa lami inayopita Ikonongo kwenda Pawaga.
Aidha akizungumzia kuhusi suala la usafi kwa manispaa hatahakikisha wanaenda kutengeneza mfumo mpya moja ni kuhakikisha mfumo wa kuzoa taka unakuwa mzuri na wakudumu ikiwezekana magari yaingie mitaani kufata taka.