
Nikiwa mwandishi na mpiga picha wa kawaida sana nisiye na makuu Novemba 27 mwaka 2011 nilikuwa mpiga picha wa matukio uzinduzi wa iliyokuwa Mall ya kisasa kabisa ya kwa kipindi hicho napengine hata sasa kama ingeendelea kuwepo lakini kwa bahati mbaya haipo tena ambayo ni Quality Centre, iliyokuwa pale Barabara ya Nyerere Jijini Dar.
Katika uzinduzi wa Mall hiyo iliyokuwa ikimilikiwa na Hayati Yusuph Manji na kusimamiwa mkewe Sukaina Manji, mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Kenya wakati huo, Raila Odinga aliyeambatana na mkewe Ida Odinga.
Wakati matukio yakiendelea nikimjua kabisa kama ndiye Raila Odinga kiongozi mwenye heshima kubwa nchini Kenya nilikuwa nikimpiga picha kiuoga nikiogopa kumkaribia.
Baada ya matukio ya uzinduzi huo kumalizika wageni wa heshima walikaribishwa kwenye lounge ya kisasa iliyokuwa kwenye Mall hiyo kwa ajili ya kujipumzisha.
Tukiwa kwenye eneo hilo ndipo stori za kubadilishana mawazo zilianza na hapo ndipo nilipoanza kumtambua Raila Odinga.
Aliniita akiwa amekaa kwenye sofa na mkewe Ida na kuanza kunisifia kwa jinsi alivyokuwa akiniona nikihangaika kutafuta engo mbalimbali. Huenda alikuwa akitaka kuanza na kunitoa shaka.
Kiucheshi aliniuliza aina ya kamera nnayotumia na ubora wake, maongezi yakiwa yanaendelea, nikiwa sijiamini kama nazungumza na Odinga yule, aliniuliza nnapoishi nami nilimwambia naishi Kigogo Luhanga.
Hapo ndipo alizidi kunishangaza aliponiambia anapafahamu eneo hilo la uswahilini.
Raila alisema siku za nyuma alikuwa akipitaga mitaa hiyo wakati barabara hiyo ikiwa ya vumbi (sasa lami) na kunitajia maeneo kama vile, Kigogo Mwisho, Njia Panda ya Festini, Kigogo Luhanga mpaka Mabibo Farasi siku hizi Mabibo Loyola akisema alikuwa na rafiki yake maeneo hayo ambaye alikuwa akimtembeleaga.
Kwa kitendo cha kuzungumza nami kwa dakika hizo kadhaa na kuwaacha waheshimiwa wenzake wakiongea mambo mengine nilimuona kuwa ni mtu wa ajabu sana.
Tukio hilo lilinifanya nianze kupata ‘comfidance’ na presha kuanza kunikaa sawa.
Hapo ndipo nilipomuona jamaa kuwa ni mtu ajabu sana kwa muheshimiwa kama yule kuwaacha waheshimiwa wenzake na kubadilishana mawazo nani nikiwa mpiga picha tu.
Si kama wengine wanavyopenda kusifia watu wanapotoweka kwenye sura ya dunia, ukweli ni lazima nisema jamaa nilimshangaa sana.
Makala hii kama ataisoma mke wa mjane wa marehemu Raila Odinga, Bi. Ida Odinga naamini itamkumbusha mbali sana siku ya tukio hilo.
Hata viongozi wa Quality Centre ambao wamelihifadhi albamu la matukio ya uzinduzi ule nao watakumbuka mengi sana wakiangalia albamu hilo nililowakabidhi baada ya kukamilisha kuliandaa.
Mungu ailaze roho ya marehemu Raila Odinga mahali pema peponi apumzike kwa amani. Amina.
Makala hii imeandaliwa nami Richard Bukos wa Global TV.