Na Khadija Kalili, Pwani
SERIKALI imepanga kuboresha miundombinu ya umeme na barabara katika Eneo la Viwanda la Zegereni, Mkoani Pwani, ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta ya viwanda.
mpango huo unajumuisha kufungwa kwa transformer yenye uwezo wa MVA 45, kuanzishwa kwa laini maalum ya umeme kwa ajili ya viwanda vya eneo hilo, pamoja na ujenzi wa barabara za kisasa zinazounganisha viwanda na barabara kuu.
Lengo kuu ni kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme na kuboresha mazingira ya uzalishaji.
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya viwanda hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Abubakar Kunenge amesema kuwa ,hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha maeneo ya viwanda nchini, sambamba na kuvutia wawekezaji wapya na kuongeza ajira.
“Eneo la Zegereni limekua kwa kasi na limekuwa kitovu muhimu cha uzalishaji. Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto za miundombinu zinashughulikiwa ili kuwezesha ukuaji endelevu wa viwanda,” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kunenge amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa kituo kidogo cha umeme cha Zegereni umeanza. Pia, mipango inaendelea ya kujenga laini mpya ya umeme kutoka Mlandizi hadi Zegereni na kuanzisha huduma ya gesi asilia kutoka Kituo chaUbungo hadi Chalinze ikijumuisha eneo hilo la viwanda.
Zegereni ni miongoni mwa maeneo ya kimkakati ya viwanda nchini na kwa sasa linachangia sehemu kubwa ya uzalishaji wa bidhaa za ujenzi na vifaa vingine muhimu vya viwandani. Maboresho ya miundombinu yanatarajiwa kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo RC kunenge alitembelea viwanda vitatu ambavyo ni Kiwanda cha kutengeneza mabati cha King- Lion, Kiwanda cha Rangi Esignia pamoja na kiwanda cha Nondo Dongfang Steel vyote vikiwa katika eneo la Zegereni.