Mwamvua Mwinyi-Kibaha
Oktoba 18,2025
Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani, Yusta Kaunda, amewataka wafanyabiashara kuona umuhimu wa kulitumia Dawati Maalum la Uwezeshaji siyo tu kwa ajili ya kudai kodi, bali kama fursa ya kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kikodi.
Yusta ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Simbani, iliyopo Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Amesema , katika kuhakikisha TRA inakwenda sambamba na kasi ya maboresho ya kiutendaji, imeamua kuanzisha Dawati hilo Maalum la Uwezeshaji kwa lengo la kuwapa wafanyabiashara huduma za kikodi na ushauri kwa haraka na kwa weledi zaidi.
“Dawati hili ni jukwaa la majadiliano, msaada na elimu kwa mlipa kodi, na siyo tu sehemu ya madai ya kodi kama wengi wanavyodhani.
Dawati Maalum la Uwezeshaji lilizinduliwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, ambaye aliwataka watendaji kuhakikisha huduma zitolewazo ni rafiki na rahisi kwa mlipa kodi.
Aidha, anaeleza mafanikio ya dawati hilo yatategemea jinsi linavyoweza kujenga mahusiano ya kuaminiana kati ya TRA na wafanyabiashara.
Yusta amewahimiza wafanyabiashara kuweka maslahi ya taifa mbele kwa kulipa kodi stahiki, huku wakilitumia dawati hilo kama daraja la kuimarisha ushirikiano wa kudumu kati yao na mamlaka.