Na Seif Mangwangi, Bagamoyo
Serikali imesema kuwa wanawake ndio kitovu cha uzalishaji na maendeleo ya familia na kwamba haki zao za kumiliki na kurithi ardhi zinahitajika kuwekwa mbele na kulindwa kwa nguvu.
Hayo yameelezwa jana Oktoba 17, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya siku ya Mwanamke aishiye kiijini iliyoadhimishwa katika kijiji cha Kaole katika Kata ya Dunda Wilayani humo.
“Wanawake ni wazalishaji wakuu katika jamii; wanastahiki haki kamili za urithi wa mali, hasa ardhi, kwa sababu ndio watunzaji wa familia lakini wamekuwa wakikuza uchumi kupitia shughuli mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya, hii ni haki ya kimsingi na sote tunapaswa kuilinda,” amesema.
DC Ndemanga amesema Serikali imekuwa ikifanyia mabadiliko Sheria zake mbalimbali ambazo zimekuwa hazitoi usawa kati ya wanawake na wanaume ikiwemo Sheria ya kumiliki wa ardhi ambapo hivi sasa Mwanamke anaweza kuwekwa kwenye hati Moja pamoja na mumewe.
Amesema Serikali kupitia mapato yake ya ndani, kila Halmashauri imekuwa ikitenga sehemu ya fedha kwaajili ya kukopesha makundi maalimu katika jamii ikiwemo wanawake ambapo wilaya ya Bagamoyo pekee kwa mwaka mpya wa fedha 2025 imetenga bilioni1 kwaajili ya kukopesha makundi hayo na kutoa wito kwa wanawake kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo.
Katika hafla hiyo, iliyoandaliwa na Shirika la utetezi wa Haki za ardhi nchini , Landesa kwa kushirikiana na shirika la Haki Ardhi na Miico la Jijini Mbeya, wanaharakati wa Haki za wanawake kutoka nchi 11 barani Afrika pia walishiriki na kuchangia uzoefu wao wa kimapambano.
Pamoja na wageni hao wa kimataifa, pia kulikuwa na uwakilishi mashuhuri wa wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania waliotoka katika jamii za kifugaji na jamii za watu wa asili, ikiwemo Wahadzabe.
Wakisoma risala kwa niaba ya wananchi na wadau waliohudhuria maadhimisho hayo, mwanaharakati Elimia Hatendi kutoka nchini Zimbabwe alisema kuwa wanawake barani Afrika wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi, hasa katika umiliki wa ardhi na upotevu wa mazao kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunaziomba Serikali zetu kutoa fidia kwa wanawake ambao wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali wakati wa uzalishaji ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuendelea kuhimili changamoto hizo,lakini pia kurejesha mbegu za asili ambazo zinahimili changamoto ya hali ya hewa,” alisema Hatendi.
Wakati huo huo, DC Ndemanga alitumia maadhimisho hayo kuzindua rasmi Ilani ya Haki za Ardhi za Wanawake iitwayo ‘Linda Ardhi ya Mwanamke Tanzania’ iliyotengenezwa na shirika la Landesa, ikiwa na dhamira ya kuendeleza juhudi za kuhakikisha wanawake wote Tanzania, bila kujitenga na asili yao, wanastahiki kumiliki na kurithi ardhi kwa usalama na heshima.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Programu kutoka shirika la Landesa, Khadija Mrisho amesema shirika hilo limekuwa likipambana kuhakikisha wanawake wanapata haki zao za msingi bila kuonewa na kwamba maadhimisho hayo ni sehemu ya kampeni hizo.
Amesema maadhimisho hayo ambayo yanafanyika kwa mwaka wa tano tangu yalipoasisiwa mwaka 2020 yamekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono jitihada za shirika hilo lakini pia Serikali kusikia sauti za wanawake na kufanyia mabadiliko baadhi ya Sheria kandamizi.
” Landesa tunajivunia mambo makubwa ambayo tumekuwa tukiyafanya kuhakikisha Sheria za kumiliki ardhi kwa wanawake zinafanyiwa mabadiliko, lakini Serikali zetu kutambua Mwanamke kama mzalishaji mkuu katika jamii, maadhimisho ya mwaka huu tumekuja kuyafanyia hapa kijiji cha Dunda Kwa kuwa ni kijijini na kina wanawake ambao ni wazalishaji, ” amesema.
Mkurugenzi wa shirika la MIICO, Catherine Mulega ambae pia ni mwakilishi wa mashirika yanayofanya utetezi wa Haki za ardhi na wanawake ukanda wa nchi za SADC ametaja nchi ambazo wanaharakati hao wametoka kuwa ni pamoja na Namibia, Eswatini, Lesotho, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Mauritius, Madagasca, Msumbiji na Tanzania.
Wanawake waliohudhuria katika maadhimisho hayo, kupitia vikundi mbalimbali walipata fursa ya kunyesha na kuuza bidhaa mbalimbali za kiasili walizozitengeneza kwa kutumia miti asili, huku wakieleza umuhimu wa mbegu asili zinazostahimili mabadiliko ya hali ya hewa ikilinganishwa na zile za kisasa.