Sehemu ya shehena ya mabomba kwa ajili ya mradi wa upanuzi na uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.
……….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
UJENZI wa mradi wa kuboresha huduma ya maji unaotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma(MBIUWASA) umefikia asilimia 64 ya utekelezaji wake.
Mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi zaidi ya 60,868 wa kata nane ambazo ni Ruhuwiko,Mbinga A,Betherehem,Matarawe,Lusonga,Masumuni,Mbinga B na Mbambi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mbiuwasa Mhandisi Yonas Ndomba amesema,mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd na unahusisha ujenzi wa vyanzo viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 1,613,200 za maji,ujenzi wa matenki manne ya ujazo wa lita 525,000 na kujenga mtandao wa bomba wenye urefu wa kilometa 57.
Ndomba amesema,mradi huo utakapokamilika,utaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kutoka asilimia 69 ya sasa hadi kufikia asilimia 90 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Ndomba amesema, mzabuni wa bomba ameshaleta kwa asilimia 95 na mkandarasi wa ujenzi anaendelea na kazi ya kuchimba mtaro ili kufikisha maji kwenye tenki na kazi hiyo imefikia asilimia 15.
Amesema,usambazaji wa maji katika Mji wa Mbinga kwa sasa ni asilimia 69 na uzalishaji wa maji ni lita za ujazo 3,200 wakati mahitaji ni lita 3,800 hivyo kuna upungufu wa lita za ujazo 600.
Kwa mujibu wa Ndomba,baada ya mradi huo kukamilika mgao wa maji katika Mji wa Mbinga utamalizika kabisa na Wananchi watapata huduma ya majisafi na salama kwa muda wa masaa 24.
Amesema,wanaaendelea kumsimamia Mkandarasi aweze kukamilisha kazi hiyo haraka ili Wananchi wa Mji wa Mbinga waweze kuondokana na mgao mkubwa wa maji na ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutenga fedha na kutoa kibali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Mbinga,wamemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili akamilishe kazi kwa wakati na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama ambayo kwa sasa ni changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Mbinga.
Joyce Kapinga mkazi wa mtaa wa Tangi la Maji A amesema, mgao wa maji ni changamoto kubwa kwani wanakaa kati ya siku tatu hadi 4 bila kupata huduma ya maji hivyo kupelekea wakati mwingine kwenda mto Luwahita kuchota maji ambayo sio safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Kapinga amesema,wakati mwingine changamoto ya maji inasababisha hata Watoto wao kwenda shule wakiwa wachafu kwa kuwa wanashindwa kufua sale au kuoga asubuhi wanapotakiwa kwenda shule ili kuwahi vipindi vya masomo.
Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji, kuanza kutekeleza mradi huo kwani wana imani kubwa baada ya mkandarasi kuanza kuleta mabomba ya kusambaza maji na shughuli za ujenzi wa mradi huo zikiendelea kufanyika.
Philomena Nchimbi amesema, la maji linasababisha hata shughuli zao za maendeleo kusua sua kwani muda ambao wanatakiwa kushiriki shughuli zao wanatumia kwenda maeneo mengine kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani.
Janifer Komba mkazi wa mtaa wa Tangi la Maji,ameishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Mbinga(Mbiuwasa)kuanza kutekeleza mradi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi wa Mji wa Mbinga.
Komba,amemuomba Mkandarasi kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika haraka na wananchi wa mtaa huo na mitaa mingine ya Mji wa Mbinga wapate huduma ya maji ya uhakika na kuondokana na kero kubwa ya uhaba wa maji iliyopo hivi sasa.