Na Sophia Kingimali
Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Ocean Road Dkt Crispin Kahesa amesema kuwa ugonjwa wa saratani haubagui wala haichagui mtu, bali ni suala la muda tu, hivyo Watanzania wanapaswa kuungana kwa mshikamano katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya mwezi wa uhamasishaji kuhusu saratani ya matiti, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kati ya wanawake wawili wanaopatikana na saratani, mmoja hufariki ndani ya kipindi cha chini ya miaka mitano, hali inayohitaji jitihada za pamoja katika kuelimisha jamii.
“Saratani haichagui wala haibagui, ni suala la muda. Tunapaswa kuwa wamoja na kujitahidi kufanya uchunguzi mapema. Mwanamke anaweza kujikagua mwenyewe eneo la titi lake mara kwa mara. Ushirikiano wetu ni muhimu katika mapambano haya,” alisema.
Aidha, amewataka waandishi wa habari kutumia nafasi zao vizuri katika kupeleka elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa saratani.
Kwa upande wake, Jonson Katanga kutoka Idara ya Kinga ya Saratani katika Hospitali ya Ocean Road, alisema kuwa Watanzania hawapaswi kuwa na hofu kwani huduma za matibabu ya saratani zinapatikana nchini kwa ubora unaolingana na ule wa nje ya nchi.
“Matibabu yapo, vifaa vipo. Sasa tuna mashine za kisasa ikiwemo mashine ya 3D zinazotumika duniani kote. Tunawaomba wananchi wafike hospitalini mapema wanapohisi dalili, kwani kuchelewa kunapunguza uwezekano wa kupona,” alisema Katanga.
Alisisitiza umuhimu wa wanawake kujenga utaratibu wa kujifanyia uchunguzi kila mwezi, hasa siku ya saba baada ya kumaliza hedhi, ili kugundua mapema mabadiliko yoyote katika matiti yao.
Naye Batuli Ramadhani, shujaa wa saratani ya matiti aliyegundulika mwaka 2015, aliiomba serikali kuangalia upya upatikanaji wa dawa za saratani, akisema wagonjwa wengi hushindwa kumalizia matibabu kutokana na changamoto za gharama na uhaba wa dawa.
“Wagonjwa wengi wanapofika hospitali na kuelezwa gharama au ukosefu wa dawa, huishia kurudi nyumbani na kutafuta tiba mbadala zisizo salama, jambo linalopelekea vifo vingi. Serikali itazame hili kwa jicho la huruma,” alisema Batuli.
Kwa upande wake, Ramadhani Mussa, mkazi wa Mbezi Maramba Mawili aliyeanza matibabu ya saratani mwaka 2005, alisema baadhi ya dawa husababisha athari za muda mfupi wakati wa matibabu, jambo linalowafanya wagonjwa wengi kukata tamaa.
Hospitali ya Ocean Road imeendelea kuwa kitovu cha matibabu ya saratani nchini, huku serikali ikiahidi kuimarisha huduma na kuhakikisha dawa, vifaa tiba na wataalamu vinapatikana kwa wote bila ubaguzi.