Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani, kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu huku akitoa rai kwa wananchi kujitokeza kupiga kura kwa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Octoba 20,2025 jijini Dar es Salaam ikiwa zimebaki siku 9 kuingia kwenye uchaguzi mkuu , Chalamila amesema kikao hicho kililenga kutoa taarifa ya usalama wa mkoa na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na vyombo vya dola ambavyo vimejipanga kuhakikisha amani inadumu wakati wote wa kipindi cha kampeni na uchaguzi.
“Mkoa wa Dar es Salaam upo salama. Vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Wananchi waendelee kufanya kazi, biashara na shughuli zao kwa furaha bila wasiwasi,” amesema Chalamila.
Aidha, alisema wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa wameendelea kufanya kampeni zao kwa uhuru na salama, huku akilipongeza Jeshi la Polisi kwa usimamizi mzuri wa amani katika kipindi hiki cha kampeni.
“Niwapongeze Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya kuhakikisha wagombea wote wananadi sera zao kwa uhuru na amani. Hata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) atakapofanya kampeni zake katika mkoa huu, tunawahakikishia wanachama na wafuasi wote kuwa usalama utadumishwa kama ilivyokuwa kwa vyama vingine,” ameongeza.
Chalamila aliwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, Oktoba 29, ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia kwa amani na utulivu.
“Tume huru ya Uchaguzi (INEC) imetoa miongozo ya namna ya kupiga kura. Rai yangu ni kwa wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuendelea na shughuli zenu kama kawaida,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alionya kuwa viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani vitashughulikiwa kwa nguvu zote za kisheria, na kuwataka wakazi wa jiji kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kulinda amani.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa huyo aliingilia kati mgogoro wa nyumba anaemuhusisha mjane bi.Alice Haule aliyedaiwa kutaka kutapeliwa mali yake.
“Mjane huyo amerejeshewa nyumba yake na kukabidhiwa hati halali ya umiliki kama msimamizi wa mirathi. Mtu aliyekuwa akijaribu kumpora nyumba hiyo, aitwaye Mohamed Mustafa, anatakiwa kuripoti katika ofisi yangu ndani ya siku tano, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Chalamila.
Chalamila amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya udhalimu na wizi wa mali za wananchi, akiahidi kuwa ofisi yake itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wa Dar es Salaam kuhakikisha haki, amani na ustawi vinadumishwa.