Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Rufijii
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha MapinduziCCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa ifikapo Oktoba 30 mwaka huu mnada wa korosho utaanza ili wakulima wa zao hilo wauze wapate fedha.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Rufiji leo Oktoba 20,2025 akiwa katika mkutano wa kampeni, Dk.Samia alianza kwa kuwapongeza wakulima wa korosho nchini kwani korosho za Tanzania zimeanza kuchukua nafasi nzuri duniani.
Amesema pia kuwa ili uzalishaji wa zao hilo ufanyike kwa wingi ni lazima serikali iendelee kutoa pembejeo ambazo ni mbolea, dawa na salfa.
Ameongeza Serikali imetumia fedha nyingi ili korosho izalishwe kwa wingi, kisha wapige mnada alafu fedha iingine kwa mkulima. “Nataka kuwaambia Pwani mmeweza kuongeza uzalishaji wa korosho.
“Rufiji mmeongeza uzalishaji mazao ya chakula kutoka tani 87,829 kwa sababu ya ruzuku tunazowapa na mbolea ambapo sasa mmefikia tani 112,118.”
Kuhusu mazao ya biashara, amesema wilaya ya Mkuranga uzalishaji zao la korosho umeongezeka kutoka kilo milioni 2.5 hadi kilo milioni 4.2 kwa msimu uliopita.
Hivyo amewaahidi wananchi hao kwamba mnada wa korosho utaanzaa Oktoba 30 mwaka huu baada ya kukamilika uchaguzi mkuu huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza Serikali kuendelea kugawa pembejeo kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika.
Kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani, Dk. Samia amesema mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta na mbaazi bado unaendelea.Pamoja na hayo ameaena kwamba lengo lao,mtizamo yao na shabaha yao ni maendeleo vijijini.
Kwa upande wa sekta ya ufugaji amesema Serikali imetoa chanjo kwa ruzuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo wanachanjwa kwa nusu bei lakini kuku ni bure. “Lengo letu kuangalia afya za wanyama wetu.”
Amesema Tanzania imepata soko kubwa la nyama na wanyama hai nje ya nchi hata hivyo kikwazo ni kwamba hakuna rekodi za dunia kama wanyama hao wamepatiwa chanjo au kutambuliwana.
Hivyo amesema kwasababu hiyo, Serikali imeanza kutoa chanjo hiyo ili Tanzania iingie kwenye rekodi.Pia Serikalii inatoa chanjo, kujenga majosho na minada ya mifugo kisha kutafuta masoko ikiwa ni hatua ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.