
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mkoa wa Rukwa una utajiri mkubwa wa madini ukiwemo makaa ya mawe, vito, dhahabu na shaba, huku akibainisha kuwa serikali imeendelea kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo sambamba na kuweka mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo.
Akizungumza na wananchi wa Sumbawanga Mjini kwenye viwanja vya Kizitwe leo, Jumapili Oktoba 19, 2025, Dkt. Samia amesema hadi sasa mkoa wa Rukwa una soko la madini pamoja na vituo sita vya ununuzi wa madini, na tayari wawekezaji zaidi ya kumi wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo mkoani humo.
“Mkoa wetu huu wa Rukwa una utajiri mkubwa sana wa madini… kwa sasa tuna soko la madini na vituo sita vya ununuzi, na wawekezaji takribani kumi wameonesha ishara ya kuja kuwekeza kwenye madini hapa Rukwa,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa kipaumbele kikubwa cha serikali kitapewa kwa wachimbaji wadogo hususan vijana wa Rukwa, ambao wataunganishwa kufanya kazi kwa ushirikiano na wawekezaji wakubwa wanaotarajiwa kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Aidha, amefichua kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu uwezekano wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata shaba ndani ya mkoa huo, hatua itakayoongeza thamani ya madini hayo na kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.
“Tunataka kiwanda cha kuchakata shaba kijengwe hapa Rukwa. Wanaohitaji shaba yetu wamekuja, wameona, tupo kwenye mazungumzo waweke kiwanda hapa hapa ili vijana wetu wapate ajira. Ndiyo maana tunajenga vyuo vya VETA vijana wafundishwe wakafanye kazi kwenye viwanda hivi,” amesema Dkt. Samia.