Viongozi wa Dini mkoani Mwanza wakitoa tamko la kuhamasisha uchaguzi
………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Zikiwa zimesalia siku 9 kuelekea uchaguzi mkuu October 29 mwaka huu kamati ya amani kwa kushirikiana na viongozi wa dini ya kikristo na kiislamu mkoani Mwanza wameungana kwa Pamoja kutoa tamko la kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na kuitunza tunu ya amani ya nchi.
Tamko hilo limetolewa leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 na kamati hiyo katika kongamano la amani lililowakutanisha viongozi wa dini mbali mbali na viongozi wa serikali.
Wakizungumza kabla ya tamko hilo wenyeviti wa kamati ya amani mkoani Mwanza Sheik wa mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke Pamoja na Dk Askofu Charles Sekelwa wamewasihi watanzania kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura ikiwa ni Pamoja na kuitunza amani.
Kwa upande wake waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amewasihi viongozi wa dini kuhubiri amani ikiwa ni Pamoja na kuendelea kuliombea Taifa na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na viongozi hao Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewahakikishia wananchi mkoani humo kuwa Mwanza ipo salama hivyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura October 29 mwaka huu pasipo kuwa na hofu yeyote.