Wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel wakizibua mshipa wa damu wa moyo wa mtoto uliokuwa umeziba, kwa kutumia mtambo wa Cathlab wakati wa kambi maalumu ya matibabu kwa watoto iliyomalizika hivi karibuni.
……………
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
20/10/ 2025 Watoto tisa wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio kwenye kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Upasuaji huo umefanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel.
Akizungumza na waandishi wa habari Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto, Stella Mongela alisema upasuaji huo ulifanyika kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara maalumu inayotumia mionzi kutambua na kutibu magonjwa ya moyo.
“Kambi hii imeokoa maisha ya watoto na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosubiri upasuaji. Tumetoa huduma kwa watoto wenye matundu kwenye moyo na wale wenye mishipa ya damu iliyoziba. Upasuaji huu mdogo unawasaidia kuepuka upasuaji mkubwa wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Stella.
Aliongeza kuwa miaka ya nyuma watoto wenye matatizo hayo walikuwa wakipelekwa Israel kwa matibabu, lakini sasa huduma hizo zinatolewa nchini kutokana na ujuzi na uzoefu mkubwa wa wataalamu wa JKCI.
“Upasuaji wa tundu dogo humsaidia mtoto kulazwa kwa muda mfupi, kupona haraka na kurejea nyumbani akiwa na afya njema, hivyo kupunguza gharama na usumbufu kwa familia”, alifafanua Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema watoto tisa waliowafanyia upasuaji wa moyo wanaendelea vizuri na kuna ambao wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Shirika la SACH Assa Sagi alisema ameshuhudia maendeleo makubwa katika utoaji wa huduma za moyo nchini.
“Nimeona jinsi madaktari wa JKCI walivyopata ujuzi na uzoefu mkubwa. Sina haja tena kuja na timu nzima, kwani sasa huduma hizi zinatolewa kwa ubora wa hali ya juu na madaktari wazawa”, alisema Dkt. Sagi.
Dkt. Sagi aliongeza kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Israel na Tanzania umeleta matunda chanya katika kubadilishana ujuzi na teknolojia, hivyo kukuza sekta ya afya nchini.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji kupitia kambi hiyo walishukuru kwa huduma bora zilizotolewa na wataalamu wa JKCI na SACH zilizookoa maisha ya mtoto wao na wamefarijika kuona huduma hizo zinapatikana hapa nchini bila kulazimika kwenda nje.
“Wazazi wenzangu wenye watoto wenye matatizo ya moyo, msiwaache nyumbani. Waleteni JKCI wapate huduma mapema ili kuepuka kupata changamoto kubwa zaidi”, alisema Mariam Rashid.
“Tulikuwa tunaishi kwa hofu, lakini sasa tumeona matumaini mapya. Tunawashukuru JKCI na SACH kwa moyo wa huruma na kazi nzuri wanayoifanya kwa watoto wetu”, alisema Abdallah Rashid.