*Awataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kuiheshimisha nchi
*Asema mengine wamuachie yeye,matusi dhidi yake hayamuumizi ,anawatumikia wananchi
Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
AMIRI Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania siku ya Oktoba 29 mwaka huu hakutakuwa na maandamano ya vurugu,hivyo wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi.
Amesisitiza kwamba maandamano yatakayokuwepo yatakayokuwepo siku hiyo ni ya watu kwenda vituoni kupigakura.Hakuna maandamano mengine yatakayokuwepo hapa huku akiweka wazi hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo.
Akizungumza leo Oktoba 21,2025 katika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam ambako anaendelea na mikitano ya kampeni kuomba kura ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mgombea urais kwa tiketi ya CCM amewaomba wananchi tarehe 29 mwezi huu watoke wakapige kura.
“Niwaombe tarehe 29 mwezi huu niwaombe tokeni mwende mkapigekura. Ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi hii.
“Nataka niwaambie, maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupigakura. Hakuna maandamano mengine yatakayokuwepo hapa. Hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo.
“Anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi.Niwaombe ndugu zangu twendeni mkapige kura. Baba ukitoka hakikisha umetoka na familia umekwenda kupiga kura.”
Aidha ametoa rai kwa mabalozi wao wa maeneo mbalimbali wahakikishe wanatoka na watu wao wote kwenda kupigakura. “Twendeni tukaheshimishe Chama Cha Mapinduzi. Twendeni tukaiheshimishe Tanzania. Tukapige kura kwa usalama turudi kwa usalama.
“Mengine niachieni mimi. Matusi niachieni mimi nayabeba kwa niaba yenu. Manabii wetu Bwana Yesu alisurubiwa kwa kukomboa watu kwa amri ya Mungu lakini alikuwa anafanyakazii ya watu.
“Nabii Muhammad alipigwa mpaka akatolewa meno kwa kufanyakazi ya kukomboa watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania na ndicho ninachokifanya.
“Niliapa kuilinda nchi na ndicho ninachokifanya. Niliapa kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha utu wa Mtanzania na ndicho ninachokifanya.
“Ninapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wetu wanapata elimu, afya ipo karibu na kila mtu, umeme upo, usalama upo ninachofanya ni kuheshimisha utu wa Mtanzania. “
Mgombea Dk.Samia amefafanua “Sina uchungu ndugu zangu wa kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu nafanyakazi hii. Sina uchungu hata kidogo wala sijutii. Niwaombe sana ndugu zangu tunawaomba kura.
“Kama nilivyosisitiza hata kibati cha soda hakitapasuka twendeni tukapige kura,”amesema Dk.Samia alipokuwa akizungumza kuhusu Oktoba 29 ambayo ndio siku ya uchaguzi mkuu.