Na Sophia Kingimali
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA), limetangaza rasmi kuanza kwa mtihani wa kujipima wa darasa la nne huku likitoa rai kwa vituo vyote vya mitihani pamoja na wanafunzi kuhakikisha mitihani hiyo inafanywa kwa weledi na nidhamu kwani baraza halitasita kufuta matokeo kwa udanganyifu wowote utakaojitokeza katika mitihani hiyo
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 21, 2025 Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, amesema mitihani hiyo inatarajiwa kuanza Oktoba 22 na 23 ambapo wanafunzi wa darasa la nne wapatao 1,582,140 kutoka shule 20,517 wanatarajiwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, kati yao 5,750 ni wenye mahitaji maalum, huku kwa mara ya kwanza kutakuwa na chaguzi kwenye masomo matatu — Kifaransa, Kichina na Kiarabu — kwa shule 115.
Amesema mwaka huu kuna mabadiliko kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mtaala ulioboreshwa, ambao utawezesha shule 115 kufanya masomo yenye lugha za kigeni kama chaguzi.
“Mwaka 2024 tulikuwa na masomo sita, sasa tisa, masomo mawili sanaa na mawili sayansi na matano ni lugha. Kati ya hayo matano, mawili ni lugha ‘mama’ — Kiingereza na Kiswahili — pia tatu zinazoanza mwaka huu ni Kiarabu, Kichina na Kifaransa,” alisema Prof. Mohamed na kuongeza:
“Shule 115 ambazo zimesajili kwa mara ya kwanza kufanya masomo haya, Kifaransa 48, Kiarabu 58 na Kichina tisa. Asilimia 50 ya alama zitahesabiwa katika matokeo ya mwanafunzi. Mtaala uliopo ni masomo sita.
“Ila lugha chaguzi zimeongeza idadi na kuwa tisa, pia yatahesabika kwenye alama za mwanafunzi, hivyo kujumuishwa kwenye matokeo.”
Aidha, Prof. Mohamed ameongeza kuwa mwaka huu shule 20,517 zitafanya upimaji huo, huku waliosajiliwa 1,582,140 kati yao wasichana ni 917,850 sawa na asilimia 51.69.
Prof. Mohamed alisema watahiniwa wa upimaji wa lugha ya Kiswahili ni wanafunzi 1,485,637 sawa na asilimia 93.27, huku wanafunzi 106,503 sawa na asilimia 6.73 wakitumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kujifunzia.
“Wapo wanafunzi 5,750 wenye mahitaji maalum, kati yao uoni hafifu ni 1,164; wasioona 111; uziwi 1,161; ulemavu wa akili 1,641 na ulemavu wa viungo 1,673.
“Maandalizi kwa ajili ya Upimaji wa Darasa la Nne yamekamilika, pamoja na kusambazwa kwa karatasi na nyaraka zote katika halmashauri na manispaa nchini,” amebainisha.
Prof. Mohamed amesema wasimamizi wamepewa mafunzo ya kuhakikisha vituo vya upimaji vipo salama na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.
“Wanafunzi wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati, pia dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine, kama mwongozo wa Baraza unavyoelekeza,” ameongeza.
Pia, amesema kwamba taarifa zinazoenea hasa mitandaoni kwamba matokeo ya Darasa la Saba mwaka 2025 yametangazwa si za kweli, na iwapo yakitoka vyombo vya habari vitashirikishwa na pia matokeo hayo rasmi huwekwa kwenye tovuti ya NECTA.