

ANTANANARIVO, Madagascar — Rais mpya wa muda wa Madagascar, Kanali Michael Randrianirina, amemteua Herintsalama Rajaonarivelo kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa madarakani aliyekuwa Rais Andry Rajoelina wiki iliyopita.
Kanali Randrianirina, ambaye awali alikuwa afisa mwandamizi wa jeshi, alitangaza kuchukua madaraka Jumanne iliyopita baada ya Rajoelina kushtakiwa kwa kutoroka kazini wakati wa maandamano makubwa yaliyotikisa taifa hilo. Aliahidi kurejesha utulivu wa kisiasa na kuandaa uchaguzi mpya katika muda mfupi ujao.
Tukio hilo lilikuja kufuatia hasira za wananchi kuhusu kukatika kwa umeme kwa muda mrefu na hali ngumu ya maisha, ambayo yalichochea maandamano ya kitaifa mwezi uliopita, yakigeuka harakati za kuipinga serikali ya Rajoelina.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu ya Antananarivo, uteuzi wa Rajaonarivelo ulifanyika baada ya mashauriano na Bunge la Kitaifa. Rajaonarivelo ni mtaalamu wa sekta binafsi, Mwenyekiti wa zamani wa benki ya kitaifa ya BNI Madagascar, na ana uzoefu wa kimataifa katika masuala ya uchumi na ushirikiano wa maendeleo.
Randrianirina alisema uteuzi huo una lengo la “kuunganisha taifa na kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za kiraia,” huku akisisitiza kuwa serikali yake “itaheshimu utawala wa sheria na kuelekea uchaguzi huru na wa haki.”