

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29, 2025, huku akisisitiza kuwa hakutakuwa na maandamano yoyote nchini siku hiyo.
Akizungumza leo katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia aliwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama ipo shwari, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara kuhakikisha kila Mtanzania anatumia haki yake ya kidemokrasia kwa amani.
“Ndugu zangu niwahakikishie, tarehe 29 mwezi huu, niwaombe mtoke kwa wingi mkapige kura. Ninaongea hapa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Nataka niwaambie, maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura hakuna maandamano mengine nchini, na hakuna tishio lolote la kiusalama. Anayesema hivi ni Amiri Jeshi wa nchi hii,”alisema Dkt. Samia.
Aidha, aliwataka wananchi kutokujibu matusi au kejeli za kisiasa, bali kuendelea kudumisha utulivu na amani wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Matusi yote wanayotukana, waacheni wanitukane mimi. Ninyi muende mkapige kura,”aliongeza.
Hotuba hiyo ni sehemu ya kampeni za Dkt. Samia katika jiji la Dar es Salaam, ambapo amekuwa akinadi sera na ahadi za Ilani ya CCM kwa ajili ya muhula ujao wa uongozi.
