Na Sophia Kingimali.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Uchumi wa Kidigitali (HEET) umefungua ukurasa mpya wa mageuzi katika elimu ya juu nchini, ukichochea ubunifu, utafiti na maendeleo endelevu kwa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wahariri kuhusu mradi huo leo Octoba 29,2025 Jijini Dar es salaam Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Prof.William Anangisye amesema kuwa mradi wa HEET ni dira mpya inayolenga kuandaa wahitimu wabunifu, waadilifu na wenye uwezo wa kuongoza Tanzania kuelekea uchumi wa kipato cha kati na ustawi wa kijamii, sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Kupitia mradi huo, UDSM imefanikiwa kuboresha miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha mitaala, na kuwajengea uwezo wahadhiri ili kuongeza ubora wa elimu na ufanisi wa kitaaluma. Hatua hii imewezesha chuo hicho kuendelea kuwa kinara wa mageuzi ya elimu barani Afrika, kikiongozwa na falsafa yake kuu ya “Hekima ni Uhuru.”Amesema.
Amesema Kupitia utekelezaji wa mradi huo, ubora wa elimu umeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa mitaala yenye viwango vya kimataifa na matumizi ya teknolojia ya kisasa. Mfumo wa e-learning umeongeza upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi walioko maeneo ya mbali au wanaofanya kazi.
Aidha Prof.Anangisye amesema kuwa, ushirikiano kati ya UDSM na sekta binafsi umechangia kuongeza ajira kwa wahitimu, ambapo tafiti zinaonyesha asilimia 82 ya wahitimu hupata ajira ndani ya mwaka mmoja baada ya kuhitimu. Mafanikio haya pia yameongeza hadhi ya chuo kimataifa na kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.
Ameongeza kuwa “Mradi wa HEET umeleta manufaa makubwa kwa makundi tofauti yakiwemo wanafunzi, wahadhiri, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla. Wanafunzi sasa wanasoma katika mazingira bora, wahadhiri wanapata mafunzo na fursa za tafiti, wakati sekta binafsi inanufaika kwa kupata wahitimu wenye ujuzi wa kisasa na ubunifu”,Amesema
Kwa upande wa jamii, Prof.Anangisye amesema matokeo ya tafiti na teknolojia mpya zinazozalishwa yameendelea kuleta suluhisho katika changamoto za kijamii na kiuchumi, sambamba na kuzalisha ajira kutokana na ubunifu wa ndani.
Mradi wa HEET unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa Dola za Marekani milioni 425. Lengo kuu ni kuboresha mazingira ya elimu ya juu na kuhakikisha mitaala inalingana na mahitaji ya soko la ajira.
UDSM imetengewa Dola za Marekani milioni 49.5, sawa na takribani Shilingi bilioni 121 za Kitanzania, kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2026.
Aidha Prof.Anangisye pamoja na uongozi wa chuo hicho wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya juu, wakisema kuwa uwekezaji huo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa linaloongozwa na maarifa na teknolojia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri(TEF) Deodatus Balile amekipongeza chuo hicho kwa utekelezaji wa mradi huo huku akitumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kuendelea kuandika mambo mazuri yanayofanywa na Serikali na kukemea mambo potofu yanayolenga kulichafua Taifa.