

MWANZA — Zaidi ya wanafunzi 1,500 kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Mwanza wamehudhuria kongamano maalum la vijana lililoandaliwa na Mwandishi na Mjasiriamali, Eric Shigongo, lililofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall, ambapo aliwahimiza vijana kuachana na utegemezi wa chanzo kimoja cha mapato na kujikita katika kuanzisha vyanzo vingi vya kipato.
Shigongo alisema njia bora ya kujikwamua kiuchumi ni kwa vijana kutumia ubunifu na maarifa waliyonayo kutatua changamoto zilizopo katika jamii na kugeuza fursa hizo kuwa miradi ya kibiashara.
“Ujasiriamali wa kisasa ni zaidi ya biashara; ni mtazamo wa maisha. Kila kijana ana uwezo wa kubuni vyanzo vingi vya mapato vinavyoweza kumjenga kiuchumi na kumsaidia kuchangia maendeleo ya Taifa,” alisema Shigongo.
Aidha, aliwahimiza washiriki kuendeleza nidhamu ya kifedha, kutumia teknolojia katika biashara ndogo ndogo, na kuwekeza mapato yao katika miradi yenye tija ili kujenga msingi wa utajiri endelevu.
Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu “Fursa za Uchumi Mpya wa Kidijitali kwa Vijana wa Tanzania” lililenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kujitegemea, ubunifu, na matumizi sahihi ya rasilimali walizonazo kufikia mafanikio makubwa.