………
Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude amesema kuwa,Serikali ya awamu ya sita inapambana sana katika kuhakikisha inawapa nguvu wananchi wake hivyo basi kwa sasa mara baada ya uchaguzi kupita atahakikisha kuwa wanaohitaji mikopo kutoka Halmashauri ya jiji la Arusha wananufaika.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero kwa wananchi wa kata ya Kimandolu pamoja na mafundi Gereji wa Suye.
Aidha Mkude amewaahidi wananchi hao kuwafanyia utaratibu wa kupata mkopo yenye riba nafuu mafundi gereji pamoja na wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika eneo la Mlima Suye Arusha.
Aidha amewataka mafundi gereji hao kudumisha umoja wao sanjari na kufuata masharti yote ambayo yanahitajika kisheria ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali.
“Nimewasikia kuwa mnahitaji mikopo ili mweze kujiongeza kwenye kazi zenu na mimi naomba niwambie kuwa sitawaangusha kabisa na nawaahidi kupata mkopo kwa wakati kikubwa mfuate sheria na kanuni zilizopo tu.”amesema Mkude.
Naye Mwenyekiti umoja wa mafundi Gereji Krokoni Suye,James Agustoni amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa kutatuliwa kwa haraka.
Aidha ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu, pamoja na ukosefu wa hati miliki ya eneo husika ambalo wanalifanyia kazi.
“Sisi tulianzia kazi zetu krokoni tukahamishiwa hapa na mvua zinaponyesha huwa hapa panakuwa pabaya Sana usalama wa maisha yetu yanakuwa hatarini kutokana na mafuriko ambayo yanatokea lami tunaomba Serikali iweze kutusaidia katika suala hilo”amesema James.
Naye Mwenyekiti Msaidizi wa umoja wa mafundi gereji Suye ambaye pia ni Mmiliki wa Nelson Shop, Nelson Natai amesema kuwa iwapo miundombinu itatengenezwa nakuwa rafiki kwa watumiaji itawawezesha kufanya biashara Kwa uhakika kwani wateja wengi wataweza kufika bila changamoto yoyote.
Aidha ameiomba Serikali kuharakisha mahitaji yao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.