Na Seif Mangwangi, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude amewataka madereva wote wanaoendelea kupiga kelele za vilipuzi maarufu kama ‘trampa’ kupitia pikipiki na magari kuacha mara moja kwa kuwa zimekuwa zikileta usumbufu kwa wagonjwa.
Amesema sheria kali inaendelea kutungwa na ambaye atakutwa akiendesha trumper atapigwa faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo kwa kuwa imekuwa ikihatarisha afya za wakazi wa Arusha.
“ Natangaza hapa rasmi wale wanaoendelea kupiga trampa kwenye pikipiki na magari kuwa Sheria kali inakuja na wote watakaokamatwa faini yake itakuwa si chini ya shilingi milioni Moja au kifungo,” amesema.
Aidha DC Mkude amewataka wamiliki wa garage ambazo hazijasjiliwa kisheria ndani ya Wilaya ya Arusha maarufu kama Garage Bubu kujisalimisha ofisini kwake Ili kubaini usajili wao kabla hatua kali za kisheria hazijaanza kuchukuliwa dhidi yao.
DC Mkude ambaye alikuwa akisikiliza kero za wananchi Leo Oktoba 22, 2025 katika eneo la Suye katika kijiji cha Kitiangare Kata ya Kimandolu lililotengwa na Halmashauri ya Arusha kwaajili ya mafundi wa magari amesema atahakikisha gereji Bubu zote zinaondoka mjini.
Awali wakiwasilisha kero Kwa mkuu huyo wa Wilaya Katibu wa Umoja wa mafundi gereji krokoni katika eneo Hilo la Suye Godfrey Majungu amesema wamekuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ubovu wa miundo mbinu ya Barabara wakati wa mvua na kuomba kujengewa daraja na Barabara kuwekwa lami.
Amesema kero nyingine ni ukosefu wa fedha Kwa wazee na vijana Ili kuwawezesha kuendeleza biashara zao ikiwemo kufuata spear za magari nje ya nchi kama wanavyofanya wafanyabiashara wakubwa.
Aidha wamemuomba Mkuu wa Wilaya kusaidia kuondoa tishio kutoka Kwa watendaji wa Halmashauri ya Jiji la kutaka kuwanyang’anya eneo hilo Kwa kuwa wameshakaa eneo Hilo Kwa miaka mingi lakini pia wamekuwa wakilipa Kodi na kuchangia miradi ya maendeleo.
Akijibu kero hizo, DC Mkude amewataka wananchi hao kufuata Sheria lakini pia atahakikisha kero zote zinazowakabili anazimaliza ikiwemo ya kutishiwa kunyanganywa eneo lao na halmashauri ya jiji hilo na kwamba atahakikisha wanapatiwa hati miliki ya eneo hilo Kwa umoja wao.
Kuhusu mikopo, amesema amegundua tatizo ni mafundi hao kukosa taarifa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji hivyo atawapelekea mtaalam wa kuwasaidia namna ya kupata mikopo hiyo ili wawe miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya halmashauri.
“ Mimi ni mtua wa vitendo nitahakikisha kero zenu nazitatua Kwa wakati, hili la Barabara tutawasilisha hoja yenu mahali husika na kuona namna itakavyotatuliwa, kuhusu mikopo pale Halmashauri Kuna fedha nyingi sana sema tu mmekosa taarifa, ijapokuwa zinatolewa Kwa vikundi na kama hauna vigezo bado Serikali imeingia makubaliano na benki pia huko mtapewa mikopo Kwa riba nafuu, nitawaletea mtaalam aje kuwaelimisha,”Amesema.
Mgombea udiwani kata ya Kimandolu Abraham Mollel ameisema mara baada ya kuchaguliwa kuwa diwani katika Kata hiyo, kero ambazo atakapambana nazo ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya lami eneo hilo na daraja ili kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo.
“Kipekee nawashukuru sana Mafundi wetu wa hili eneo, mmekuwa mkisaidia kuwavusha watoto wetu kwenda shule kipindi cha mvua maji yanapojaa, mtaa wetu huu una huduma muhimu za kijamii ikiwemo shule ya msingi na sekondari, kanisa lakini pia wafanyabiashara wanaoingizia taifa mapato. Naomba suala hili liangaliwe kwa jicho la pekee” amesema.
Mmoja wa mafundi hao Ibrahim Mkuruzi amesema ana imani na serikali ya awamu ya sita na anamshukuru Daktari Samia Suluhu Hassan kuwateua viongozi makini katika Jiji la Arusha.
Mbali ya kusikiliza kero za Wananchi DC Mkude ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba mwaka huu ili kuchagua viongozi bora watakaoleta maendeleo ya nchi.