
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati wote, hususan katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Akizungumza leo tarehe 22 Oktoba 2025 Jumatano katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ilala, jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia amewatoa hofu wananchi kuhusu vitisho vinavyoenezwa mitandaoni na baadhi ya watu, akisisitiza kuwa Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama.
“Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ndani ya taifa hili vimejipanga vyema, tumevijengea uwezo wa kutosha. Iwe wakati wa uchaguzi au bila uchaguzi, tupo salama wakati wote,”alisema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa vitisho vinavyotolewa na watu wachache havina msingi wowote, na kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura bila hofu ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
“Tusiruhusu woga au maneno ya kutisha kutuvunja moyo. Uchaguzi ni haki yetu, na amani ni jukumu letu sote,”
alisisitiza.
Dkt. Samia amehitimisha hotuba yake kwa kupongeza kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini, akibainisha kuwa serikali itaendelea kuviimarisha kwa vifaa na mafunzo ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kudumishwa.