
Klabu ya Yanga imetangaza kuwa mchezo wao wa mkondo wa pili wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Silver Strikers FC ya Malawi utakuwa bila kiingilio kwa majukwaa yote, isipokuwa VIP A na VIP B ambazo zimehifadhiwa kwa wageni waalikwa.
Tangazo hilo limetolewa leo Oktoba 21, 2025 na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Shaban Kamwe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo utakaopigwa Oktoba 25, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
“Mechi hii ya maamuzi ya kuipeleka Yanga hatua ya makundi ya CAF Champions League imeondolewa viingilio majukwaa yote, isipokuwa jukwaa la VIP A na VIP B ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya wageni waalikwa,” alisema Kamwe.
Ameongeza kuwa uamuzi huo umetokana na maombi ya mashabiki na wanachama wa Yanga walioomba mchezo huo uwe bure ili kutoa sapoti kubwa kwa timu yao katika mchezo wa nyumbani wa kuwania kufuzu hatua ya makundi.
“Viongozi wa klabu yetu walikutana leo asubuhi kujadili maombi ya wanachama na mashabiki wetu. Wamekubali ombi hilo, na hivyo mashabiki wote wataingia bure kwenye majukwaa yote isipokuwa VIP A na VIP B,” aliongeza Kamwe.
Aidha, Kamwe ametoa onyo kwa watu wasiokuwa mashabiki wa Yanga watakaokuja uwanjani kwa nia zisizo nzuri, akisisitiza kuwa siku hiyo ni ya wanayanga kuonesha upendo kwa timu yao.
“Ombi hili limeombwa na wanayanga kwa viongozi wao, na viongozi wameruhusu. Sasa wewe ambaye sio Yanga na ukaja Benjamin Mkapa na dhamira zako za hovyo hovyo — tutalaumiana. Kama unakuja, uje uangalie mechi na utulie,” alisema kwa msisitizo.
Yanga inahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025/26, baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Malawi.