

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Amani Golugwa, amesema hadi sasa chama hicho hakijapata taarifa rasmi kuhusu alipo Makamu Mwenyekiti wao wa Tanzania Bara, John Heche, licha ya kuambiwa na Jeshi la Polisi kuwa amepelekwa Tarime, mkoani Mara.
Golugwa ametoa kauli hiyo nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mara baada ya kuahirishwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
“Siku ya jana, Makamu Mwenyekiti wetu wakati anaingia katika geti la Mahakama Kuu hapa alikamatwa na kuwekwa katika mikono ya Jeshi la Polisi. Alielekezwa Central Police, na taarifa tulizopokea kutoka kwa Mawakili wetu zilieleza kwamba kweli walimchukua na kumpeleka Tarime, Mara.
Lakini hadi sasa, yakiwa yamepita zaidi ya masaa 24, tumefuatilia Wilayani Tarime na Mkoani, Mawakili wameenda kuuliza iwapo Heche amefikishwa, lakini tumeambiwa hajafikishwa,” alisema Golugwa.
Kwa mujibu wa Golugwa, chama hicho kimeendelea kufuatilia kwa karibu ili kubaini hatua alizopitia kiongozi huyo tangu alipokamatwa jana asubuhi akiwa anaingia kwenye viunga vya Mahakama Kuu.