Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya sita imefanya kazi kubwa kusimamia utawala bora na kwa sasa hakuna haki ya mtu inayopotea kwa sasa.
Akizungumzia Oktoba 22,2024 akiwa katika mkutano wa kampeni wa kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu Dk.Samia pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuelezea utawala bora nchini.
Akifafanua mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ,Dk.Samia katika masuala ya utawala bora, Serikali iliunda Tume ya Haki Jinai kuangalia namna haki za wananchi zinavyopatikana.
Amesema kwamba tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake iliwasilisha serikalini taarifa ambapo sasa sekta ya haki na sheria ipo vizuri.
“Haki za watu sasa hazipotei kama ilivyokuwa, sasa hivi polisi, mahakama, DPP, DCI wote wanasomana. Ule mchezo wa ndugu zetu kwenda kuweka maneno kwenye taarifa alizosema mtu sasa hivi haupo,” amesema Dk.Samia.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya kutolea haki nchini kwa kuboresha mahakama za wilaya, mikoa na jumuishi.
Pia amesema kuwa tume ya pili aliyoiunda ni tume ya kuangalia uhusuano wa Tanzania kimataifa.”Baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake, Tanzania imefanikiwa kurejesha heshima yake kimataifa.
“Tume nyingine ni ya kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo iliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro.Baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake, kila jambo linalofanywa na serikali linazingatia mahitaji ya dira ya taifa.”
Ameongeza pia serikali yake iliunda tume nyingine maalum kuangalia masuala ya kikodi nchini ambapo tume hiyo imemaliza kazi wakati tunaingia kipindi cha kampeni.”Kwahiyo wataleta taarifa yao baada ya kuunda serikali mkitupa ridhaa yenu.”
Mgombea urais Dk.Samia amesema kwamba baada ya kuunda serikali italeta taarifa yake na tutafanya mageuzi ya kodi Tanzania lakini maoni yote wameyapata kwa wananchi.
Dk.Samia amesema tume nyingine iliyoundwa ni ya kuangalia mgogoro uliopo Loliondo ambayo nayo imeshakamilisha kazi yake hivyo baada ya uchaguzi itawasilisha taarifa kisha hatua stahiki zitachukuliwa.
“Tume zote hizo zimezingatia maoni ya wananchi hatua ambayo inathibitisha uwepo wa utawala bora nchini.Hakuna anayejua kila kitu, ukitaka kuendesha nchi kwa amani lazima uwashirikishe wenye nchi na ndiyo demokrasia.
Amesisitiza kwamba “Tunafanyakazi kwa ajili ya watu na hao watu ndiyo wenye mpini wa kuendesha nchi na siyo watawala wenye mpini wa kuendesha nchi hii.”
Ameongeza Serikali yake imeboresha majengo yanayotoa huduma kwa wananchi ambapo watu wenyeulemavu wanaweza kufika kupata huduma kwa urahisi.
Wakati huo huo amesema kwa upande wa halmashauri, Serikali imejenga majengo 126 ya halmashauri mbalimbali nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Amefafanua ofisi zilikuwa mbali na wananchi lakini kwa sasa maofisa wa serikali wa sekta zote wako karibu.”Anayeshughulikia kilimo yupo hapa, maji yupo kule lakini sasa huduma zote zinapatikana ndani ya jengo moja na ni majengo ya heshima kwelikweli.
Pia amesema katika kumpa raha mwananchi, mawasiliano ni muhimu hivyo Serikali imetenga fedha kujenga minara zaidi ya 700. “Lakini mpaka sasa tunavyozungumza tumejenga minara zaidi ya 600.”