

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya vizuri katika kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa furaha, amani na uhuru.
Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Tanesco, Buza, Wilaya ya Temeke, Dkt. Samia amesema serikali yake imeweka mazingira mazuri yanayowawezesha wananchi kufurahia maisha yao bila hofu, huku ikihakikisha haki na huduma muhimu zinapatikana kwa wote.

“Kama unakaa pazuri, unakula vizuri, afya nzuri, maji unayapata, umeme unauona, ukipata kuwasha TV unawasha — maana yake furaha ipo. Ukihitaji haki yako unaipata, michezo unacheza, kwa hiyo katika eneo la furaha tumefanya vizuri na tunajipanga kufanya vizuri zaidi,” alisema Dkt. Samia.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, uhuru wa maoni na kujumuika umeimarika kwa kiwango kikubwa, huku serikali ikiendelea kuzingatia mila na desturi za Mtanzania.
Aidha, Dkt. Samia amesema serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya michezo, muziki na sanaa, ambazo zimekuwa chanzo cha ajira na kipato kwa vijana wengi nchini.
Pia alisisitiza kuwa serikali imeendelea kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu, wakiwemo watu wenye ualbino, kwa kuhakikisha usalama wao na kuwahusisha kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Leo tunashuhudia walemavu wakijumuishwa katika maendeleo. Wana nafasi sawa kama wengine. Hii ndiyo Tanzania tunayojenga – yenye furaha, amani na fursa kwa wote,” aliongeza Dkt. Samia.
Kwa mujibu wa mgombea huyo wa CCM, serikali yake itaendelea kusimamia sera za maendeleo jumuishi na kuimarisha huduma za kijamii kwa wananchi wote bila ubaguzi.