MAHAKAMA Kuu masjala ndogo ya Dar es salaam imekubaliana na pingamizi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu la kuzuia vielelezo vya upande wa Jamhuri kuingia kwenye kesi ya uhaini inayomkabili.
Awali Lissu alitoa pingamizi akimpinga shahidi huyo kuwasilisha taarifa ya uchunguzi kama kielelezo akidai kuwa shahidi aliyeletwa na upande wa Jamhuri hana sifa za kisheria kuwasilisha ushahidi huo mahakamani.
Aidha, Mahakama hiyo imesema kwa msimamo wake haikubaliani na Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema kwamba kuna mtego sehemu yoyote na pia haiwezi kuingia kwenye mtego wa kukiuka sheria.
Uamuzi huo mdogo umetolewa Oktoba 23,2025 na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na kukubaliana na pingamizi zilizowasilishwa na Lissu.
“Shahidi huyu, licha ya kuwa ofisa mwenye taaluma ya uchunguzi wa picha, hakuteuliwa kama mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (cyber expert) bali alipewa jukumu maalum la kuchunguza na kuhakiki picha mnato zilizowasilishwa kwake kwa maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),” amesema Jaji Karayemaha.
Jaji Karayemaha amebainisha kuwa majukumu ya shahidi huyo yamefafanuliwa wazi katika Tangazo la Serikali (GN) namba 779 la mwaka 2020, mamlaka yake yanahusiana na uchunguzi wa picha na kuandaa cheti cha uhakiki (certificate) baada ya uchunguzi, siyo kuandaa ripoti ya kitaalamu (expert report) kama ambavyo ilifanyika katika kesi hii.
“Shahidi huyu alikuwa na wajibu wa kuandaa cheti cha uthibitisho wa picha baada ya uchunguzi wake, lakini badala yake aliwasilisha ripoti ambayo kisheria haiwezi kutumika kama ushahidi wa kitaalamu,” amesema Jaji Karayemaha.
Pia, Mahakama imekubaliana na hoja za Lissu kupinga kupokelewa kwa taarifa hiyo kwa maelezo kwamba vyombo vilivyodaiwa kuhifadhi picha mjongeo, ikiwemo flashi disk na kadi ya kumbukumbu, vilishakataliwa na Mahakama, hivyo hakuna msingi wa kupokea taarifa inayohusiana navyo.
Amesema kwa kuwa vifaa hivyo vilivyodaiwa kuwa chanzo cha picha havikukubalika kama vielelezo, hakuna sababu ya kupokea taarifa yoyote inayotokana navyo. Hivyo, kielelezo hicho hakiwezi kupokelewa.
“Tunakubaliana na mshtakiwa kutokana na vifaa hivyo kukataliwa, hiyo taarifa inaenda kuelezea nini, tunaipokea kufanya nini, ndiyo maana tunasema tukiwa tunaongozwa na kesi ya Jamhuri dhidi ya Sharifu Mohamed huyu shahidi hana uwezo wa kutoa hii taarifa.
“Kwa hiyo tunaona pingamizi la mshtakiwa lina mashiko na sisi hatutaipokea hiyo taarifa ambayo walitaka kuitoa kupitia shahidi namba tatu,” amesisitiza Jaji Karayemaha.
Pia, amesema wakati Wakili Mrema anawasilisha hoja zake alizungumzia suala la Mahakama kuingia kwenye mtego wa mshtakiwa kutokana na pingamizi alizoziwasilisha.
“Kwa msimamo wa Mahakama hatukubaliani na Wakili Mrema kwamba kuna mtego sehemu yoyote na sisi hatuwezi kuingia kwenye mtego wa kukiuka sheria,” amesema Jaji Karayemaha.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Mahakama imeridhia pingamizi lililowasilishwa na Lissu na hivyo kutupilia mbali kielelezo hicho, ikibainisha kuwa shahidi husika hana sifa za kisheria za kutoa taarifa ya uchunguzi wake kama kielelezo katika kesi hiyo.
Awali, Wakili Mrema alidai kuwa pingamizi la mshtakiwa halina mashiko na pia Mahakama hiyo haifungwi na uamuzi wake uliotoa kuhusu flash disks na kadi ya kumbukumbu (memory card).
“Mshtakiwa alienda mbali kwa kuingilia maudhui ya ripoti na kuanza kuzisoma na kwamba hilo lilishakataliwa na Mahakama ya Rufaa, kielelezo kinatakiwa kiwe safi ndiyo kisomwe, kwa hiyo ni kinyume na sheria,” alidai Wakili Mrema.
Baada ya uamuzi huo, Lissu alipewa nafasi ya kumuuliza shahidi maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliyoutoa mahakamani wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Thawabu Issa.
Lissu alisoma maelezo yote ya shahidi na kumsomea shahidi maneno 75 ambayo anataka kumuhoji ili ayakanushe, ikiwemo eneo la elimu ya shahidi huyo.