Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu na Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa hospitali hiyo Iddi Lemmah wakimsikiza CPA. Cosmas Mbogela wakati akitoa mafunzo ya jinsi ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.

Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group wakimsikiza CPA. Cosmas Mbogela wakati akitoa mafunzo ya jinsi ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam. (Picha na JKCI)
………..
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wanahudhuria mafunzo ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa mpango mkakati unaolenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuhakikisha maendeleo ya kiutendaji hayaathiriwi na changamoto zinazoweza kuzuilika kupitia mipango thabiti.
Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo alisema mafunzo hayo yataisaidia hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma bora salama na endelevu kwa wananchi.
“Leo tumejifunza namna ya kubaini vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira yetu ya kazi iwe ni katika utendaji wa kila siku au katika hatua za maendeleo ya taasisi. Mafunzo haya yatasaidia kuhakikisha tunabaki kwenye mstari wa mafanikio na kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Dkt. Shemu.
Aliongeza kuwa JKCI Hospitali ya Dar Group inahudumia wastani wa wagonjwa 500 kwa siku, na katika kipindi cha miaka mitatu imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma bora za moyo na magonjwa mengine kwa kuzingatia miongozo ya kisera na bajeti ya mwaka ambayo inaelekeza utekelezaji wa shughuli.
“Azma yetu ni kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila mtanzania kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumejipanga kutoa huduma za kiwango cha juu hapa nchini na kuvuka mipaka ya nchi”, alisisitiza Dkt. Shemu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa hospitali hiyo CPA. Ashura Ally alisema uandaaji wa rejesta ya vihatarishi ni takwa la Wizara ya Afya ambapo kila taasisi ya umma inapaswa kuandaa rejesta hiyo ili kuimarisha utendaji wake.
“Tumepata mafunzo ya jinsi ya kutambua viashiria vya vihatarishi, namna ya kuviainisha, kuvipangia mikakati ya kudhibiti na kuviingiza kwenye mipango ya bajeti. Hii itatusaidia kuhakikisha taasisi haikwami katika utendaji wa kila siku bali inaendelea kufanikisha malengo iliyojiwekea”, alisema CPA. Ashura.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa JKCI hospitali ya Dar Group Iddi Lemmah alisema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo kwani yamewasaidia kuelewa namna bora ya kuendesha taasisi kwa ufanisi.
“Tumejifunza namna ya kuainisha vihatarishi vinavyoweza kuchelewesha au kuzuia utekelezaji wa malengo ya taasisi pamoja na kuweka mikakati ya kuvithibiti na kuandaa bajeti ya kukabiliana navyo”, alisema Lemmah.
JKCI Hospitali ya Dar Group inatoa huduma za matibabu ya moyo, kinywa na meno, matibabu ya magonjwa ya kuambukiza kama malaria, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, kliniki ya macho, pua, masikio na koo, kliniki ya mfumo wa mkojo, matibabu ya magonjwa ya tumbo na ini, figo, huduma za baba, mama na mtoto (RCH), upasuaji mkubwa na mdogo, upimaji wa VVU na ushauri, fiziotherapia (mazoezi tiba), huduma za maabara na gari la wagonjwa.









