*TARURA Ruvuma kutekeleza Miradi ya Bilioni 22 kwa mwaka 2025/2026
Ruvuma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Ruvuma umeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya barabara, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi, kilimo, na uhifadhi wa mazingira.
Meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo, amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, mkoa huo unatekeleza miradi ya maendeleo yenye bajeti ya shilingi bilioni 22, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka bilioni 7 za awali.
“Kwa sasa, TARURA Ruvuma inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 7,147, ambapo kilomita 133.69 ni za lami, 1,651.8 ni za changarawe, na 5,360.6 ni za udongo. Takribani asilimia 70 ya barabara hizo zinapitika msimu wote, jambo ambalo limeleta mabadiliko chanya kwa wakulima na wafanyabiashara wa mkoa huo”.
“Barabara hizi zimekuwa mkombozi kwa wakulima. Mazao kama mahindi na kahawa sasa yanafika sokoni kwa wakati, bila kuharibika njiani na hivyo kuongeza uchumi kwa wakulima”, amesema Mhandisi Chinengo.
Aidha, Meneja huyo amesema TARURA imefanya manunuzi ya mikataba 43 yenye thamani ya shilingi bilioni 12.1, na iko katika hatua za mwisho za kusaini mikataba hiyo.
Ameongeza kusema kwamba kwa mwaka uliopita pekee, zaidi ya kilomita 3 za barabara za lami zimejengwa, na taa za barabarani zimewekwa ili kuongeza usalama na mwonekano wa mji kwa usiku.
“Kwa sasa, kila barabara inayojengwa inaambatana na uwekaji wa taa hatua inayoongeza usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi hasa nyakati za usiku.
Katika kulinda mazingira, Mhandisi Chinengo amewataka wananchi kutotupa taka kwenye mitaro ya maji na kushiriki katika utunzaji wa miundombinu.
“Serikali imewekeza fedha nyingi ni jukumu letu kuhakikisha barabara hizi zinadumu kwa muda mrefu kwa kuepuka uharibifu wa makusudi,” amesisitiza.
Naye, Bi. Eva Ndomba mkazi wa Makambi amesema awali barabara zilikuwa na nyasi, vumbi na hata pikipiki zilikuwa zinapata changamoto kupita ila wanaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara za lami kwani wanapita vizuri na uwekaji wa taa umewasaidia kwa sasa wanafanya biashara hata usiku.
Wakati huo huo, Bw. Ally Musa ambaye ni mkazi wa Makambi amesema wanashukuru kwa ujenzi wa barabara ya lami awali hususan kipindi cha masika walikuwa wakipita vichochoroni lakini sasa wanakatiza kwenye barabara na uwekaji wa taa wao kama vijana zimewasaidia kufanya shughuli zao hadi usiku.










