

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahimiza vijana wa Tanzania kutodanganywa na mitazamo kuhusu maisha ya nje ya nchi, akisisitiza kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa bora zaidi barani Afrika kwa fursa na ustawi wa wananchi wake.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Alhamisi, Oktoba 23, 2025, katika Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia alisema Tanzania ni nchi yenye heshima, jina kubwa na inayowathamini watu wake, hivyo vijana hawapaswi kukatishwa tamaa na taarifa zisizo sahihi kutoka nje.
“Nataka kuwahakikishia vijana wa Kitanzania, msidanganywe. Ukichukua Afrika Mashariki, pengine na Kusini na Kati mwa Afrika, Tanzania ni pepo. Hapa mpo kwenye nchi yenye jina, yenye sifa zake na yenye kuendeleza watu wake,” alisema Dkt. Samia.

Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kutambua kuwa wao ndio warithi wa taifa, na kwamba serikali ina imani kubwa nao katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
“Sisi wazazi wenu tunapita, nchi hii inawategemea ninyi. Tunatarajia tuwaachie nchi muiendeshe kama tunavyoiendesha sisi. Msidanganywe hata kidogo, hii nchi ni mali yenu, si ya mwingine,” alisisitiza.
Aidha, aliwaonya vijana kutojihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, akiwataka kuendelea kufuata sheria, Katiba na maelekezo ya serikali.
“Niwaombe msiharibu amani ya nchi yenu. Fuateni serikali yenu inavyowaelekeza, fuateni Katiba yenu inavyowaelekeza, fuateni sheria za nchi zinavyotaka, mtaishi kwa salama na amani,” alisema Dkt. Samia.









