Na Khadija Kalili, Pwani
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imekabidhi hundi ya Sh.bilioni 2.1 kwa wafanyabiashara wadogo waliopo katika Halmashauri hiyo ikiwa ni fedha za makusanyo ya mapato ya ndani ya asilimia 10 kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu.
Hundi hiyo inekabidhiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt . Roger’s Shemwelekwa jana Oktoba 23/2025 mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya wafanyabiashara hao yaliyokuwa yakifanyika kwenye Ukumbi wa Kibaha Shopping Mall uliopo karibu na Stendi Kuu ya mabasi yaendayo Mkoani.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hundi hiyo Shemwelekwa amewaomba wajasiriamali hao kutumia vizuri fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Dkt.Shemwelekwa amesema kuwa fedha zinazotolewa ni makusanyo ya mapato ya ndani ambapo yameongezeka kutoka Bilioni 8 hadi kufikia bilioni 21 ya mwaka ulioisha.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaelekeza wao kama viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanawawezesha wafanyabiashara wadogo ili kuinua biashara zao.
Amesema wapo wafanyabiashara wengine wanashindwa kuendeleza biashara zao kwa kukosa mitaji kwahiyo Halmashauri imekuja na mpango wa kuhakikisha kila mfanyabiashara mdogo anainuliwa kiuchumi kupitia mikopo ya Halmashauri.
Shemwelekwa amewaomba wafanyabiashara hao kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati na wale ambao watarejesha kwa haraka watakuwa wanapewa mikopo mingine papo hapo.
Ameongeza kuwa anataka kuona wafanyabiashara wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wananeemeka na Halmashauri yao kwa kuhakikisha kila mmoja anakua kiuchumi ili ifike mahali wawe na viwanda vyao.
Amesema kwasasa wanawaondolea hadha ya kwenda kukopa mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa ikisababisha biashara zao kufa na kuwasisitiza kukopa mikopo ya Halmashauri ambayo haina riba.
Amesema vipo vikundi ambavyo vinatumia vizuri fursa ya mikopo hiyo akitolea mfano wa kikundi cha wajane kilichopo Kata ya Kongowe ambacho msimu ulioisha kilipata Sh.milioni 49 na walifanikiwa kurejesha vizuri na msimu wameomba milioni 200 na watapata kwakuwa wamekuwa waaminifu.
“Ninawaahidi kuwapa hela za kutosha endapo mkirudisha kabla ya wakati kwakuwa naamini tukiwawezesha wajasiriamali uchumi wa Kibaha utakua na maendeleo yatapatikana kwa mtu mmojammoja,”amesema Dkt .Shemwelekwa.
Amesema anataka kuona Kibaha inabadilika na wafanyabiashara wapate fursa ya kufanya biashara zao hadi usiku wa manane bila kusumbuliwa na Polisi na kwamba tayari amezungumza na Polisi kuacha kuzuia watu kufanya biashara.
Amesema ,kazi ya askari wa Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao lakini pia kudumisha amani na usalama na sio kukamata wafanyabiashara kwahiyo waende wakafanye biashara zao bila wasiwasi.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Leah Lwanji amesema kuwa kabla ya mkurugenzi huyo kukabidhi hundi hiyo kulikuwa na Mafunzo maalum ya wajasiriamali wapatao 3600.
Lwanji amesema kuwa wafanyabiashara hao ni sehemu ya robo ya kwanza ya Mwaka 2025/2026 ambapo jumla ya fedha zilizotolewa ni Sh.bilioni 2.1 kukiwa na wanufaika 3,300 na vikundi 660.
Lwanji ,amesema kuwa idadi ya fedha hizo imeongezeka kwani katika kipindi cha robo ya mwaka wa 2024 /2025 fedha zilizotolewa zilikuwa Sh.milioni 956.17 kwa wanufaika 485 kupitia vikundi 97.
Nao wajasiriamali wa mikopo hiyo akiwemo Hassan Forodha na Kaiche wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kupitia mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa namna ambavyo amejitoa katika kusaidia wafanyabiashara wadogo.
Wamesema kuwa,kufuatia hali hiyo watakuwa mabalozi wa wenzao katika kuhakikisha mikopo waliyopewa wanakwenda kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa hususani katika kuendeleza mitaji ya biashara zao.










