NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema mkoa huo umejipanga vyema kuhakikisha amani na utulivu vinatawala siku ya kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu, ili wananchi waweze kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa utulivu bila usumbufu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, RC James alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama na tulivu, hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kupiga kura bila hofu.
Alisema kuwa hali ya usalama mkoa wa Iringa iko vizuri na wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 na kuondokana na vitisho kwani serikali iko makini na jeshi la polisi limejipanga vyema kulinda raia na mali zao siku hiyo.
Vilevile alisema kuwa siku ya Oktoba shughuli za umma zitaendelea kama kawaida wafanyabiashara waendelee na biashara huduma za afya zinaendelea kasoro shule na huduma za serikali ambazo hazihusiani na uchaguzi.
“Wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida, hakutakuwa na changamoto yoyote itakayoathiri upigaji kura, wala huduma zote muhimu za kijamii zitaendelea kutolewa kama kawaida,” alisema
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha mshikamano na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani, huku akitoa onyo kali kwa watu watakaobainika kupanga au kujaribu kuvuruga utulivu wa mkoa huo.
“Natoa onyo kwa yeyote mwenye nia ya kuvuruga amani, vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara, makini na tayari kuchukua hatua stahiki dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Iringa itaendelea kushirikiana na taasisi zote za ulinzi na usalama kuhakikisha kila raia anashiriki katika zoezi la upigaji kura kwa uhuru na amani.
Aidha alisema kuelekea katika uchaguzi mkuu wananchi wanatakiwa kufata maelekezo ya tume huru ya uchaguzi ili waweze kufahamu mengi yanayotolewa na tume hiyo.







