Kassim Nyaki, NCAA.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Jenerali Venance Mabeyo (Mst) amewavisha cheo makamishna wasaidizi waandamizi wa uhifadhi wawili na kuwahimiza Kuchapa kazi, uadilifu, kutimiza wajibu, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji kazi katika utumishi wa Umma.
Waliovishwa Cheo baada ya kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Brown O. Shimwela anayesimamia Idara ya fedha pamoja na Kamishna msaidizi Mwandamizi Dkt. Amani Makota anayesimamia Idara ya TEHAMA na Takwimu.
Baada ya kuwavisha vyeo Jenerali Mabeyo ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi Mstaafu amewasisitiza viongozi hao wapya kushirikiana na Menejimenti ya Ngorongoro kuboresha zaidi miundomninu ya utalii, kuboresha huduma kwa wateja, kubuni mazao mapya ya utalii, na kusimamia kikamilifu maeneo ya malikale yaliyopo nje ya eneo la Ngorongoro kama Mapango ya Amboni na Kimondo cha Mbozi ili rasilimali hizo za malikale ziongeze mchango katika pato la taifa.
“Tuboreshe huduma za wageni ikiwemo miundombinu ya utalii, vivutio vya malikale kama mapango ya ambone na Kimondo cha Mbozi, tubuni mazao mapya ya utalii, kuyaendeleza na kuyatangaza ili kuwe na mtawanyiko wa wageni wanaotembelea hifadhi, uboreshaji wa miundombinu uende sambamba na kuimarisha mifumo ya TEHAMA iendelee kusomana kwa ajili kuongeza kwa Taifa letu na watanzania kwa Ujumla” amesisitiza Mabeyo
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru ameleza kuwa makamishna hao wapya kuungana na Menejimenti ya Ngorongoro ni sehemu ya kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa majukumu ya kusimamia Uhifadhi, utalii na Maendeleo ya Jamii kikamilifu katika kukuza uchumi wa Nchi.
Badru ameongeza kuwa Utalii ni sekta kinara katika kuchangia uchumi ya Nchi, hivyo mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Wadau wa utalii inaendelea kuongeza mazao mapya ya utalii na kuyatangaza ili kuongeza idadi ya watalii na pato la taifa.










