Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Kaya ishirini na nane (28) za maeneo ya Msasani Maisaka A na Maisaka Kati Wilayani Babati, mkoa wa Manyara zalipwa fidia ya bilioni 2.9 baada ya maeneo yao kutwaliwa na Serikali kwa matumizi ya huduma za Kijamii. Taarifa ya malipo ya fidia hiyo zilitolewa na Mkuu wa mkoa kupitia kikao kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa mkoa, Oktoba 23, 2025.
Kupitia kikao hicho wananchi hao walimshukuru Mhe. Queen Sendiaga Mkuu wa mkoa wa Manyara wa kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu malipo ya fidia ya maeneo yao hayo. Walieleza kuwa wamekaa muda mrefu tangu mwaka 2008 pasipo kujua hatma yao. Hivyo walishukuru uongozi wa Serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kukata kiu yao ya muda mrefu.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga aliwashukuru na kuwapongeza wananchi hao kwa kuridhia kuyaachia maeneo hayo ya vyanzo vya maji kwa manufaa ya jamii nzima ya wakazi wa Wilaya ya Babati ambao hutegemea chanzo hicho.
Vile vile amewataka wananchi hao kuridhika na kiwango kilichotolewa na Serikali Baada ya kufanyika kwa tathmini ya mwisho mwaka 2024.
Huku akiwaahidi kuwapatia viwanja vya Bei nafuu vilivyopimwa lakini aliwasihi wananchi hao kutumia fedha hizo za fidia kujenga makazi mapya na kujiendeleza kiuchumi.
Mwisho , Mhe. Sendiga ametoa muda wa miezi sita wananchi hao waweze kuondoka kwa hiari kwenye maeneo hayo ili Mamlaka ya Maji Babati (BAWASA) waanze kutekeleza mradi mkubwa wa usambazaji wa maji katika Mji wa Babati.








