Dar es Salaam, 24 Oktoba, 2025 Mchana:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa
Kimbunga “CHENGE” katika Bahari ya Hindi, Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha
Madagascar.
Kimbunga “CHENGE” kimeendelea kusalia baharini na kusogea kuelekea Magharibi, yaani
kuelekea pwani ya nchi yetu. Hadi kufikia asubuhi ya leo Kimbunga “CHENGE” kilikuwa katika
eneo la Bahari ya Hindi umbali wa takribani kilometa 1,680 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa Kimbunga hicho kinatarajiwa
kuendelea kusogea kuelekea Magharibi zaidi mwa Bahari ya Hindi ulipo ukanda wa pwani wa
nchi yetu huku kikipungua nguvu yake kadri kinavyosogea. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha
uwezekano mdogo wa vipindi vya ongezeko la mvua, upepo na mawimbi makubwa ya Bahari
kati ya tarehe 26 hadi 28 ya Mwezi Oktoba, 2025 hususan kwa maeneo ya mikoa ya Mtwara,
Lindi, Pwani, Dar es salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga
“CHENGE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa
kila inapobidi.
USHAURI: Watumiaji wa Bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea
kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.







