Na Silivia Amandius
Kagera:
Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Anastaz Mpanju, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wengine ili kuwaleta wananchi pamoja na kuwapatia elimu kuhusu namna ya kutumia rasilimali zao kwa maendeleo endelevu.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki kwa maafisa maendeleo ya jamii katika mkoa wa Kagera, Mpanju alisema maendeleo ya kweli yapo kwa wananchi, hivyo ni muhimu watumishi hao kuwafikia hadi ngazi za vijiji.
“Maendeleo yapo kwa wananchi. Ili wayaone ni lazima tuwafikie hadi ngazi za chini, ndiyo maana serikali inaendelea kutoa nyenzo kama hizi pikipiki ili kurahisisha kazi ya kuwafikia wananchi,” alisema Mpanju.
Katika hafla hiyo, pikipiki 9 zenye thamani ya shilingi milioni 33.8 zilikabidhiwa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri nne za mfano ambazo ni Ngara, Missenyi, Karagwe na Bukoba Vijijini.
Mpanju aliwataka maafisa hao kushirikiana na watumishi wengine wa serikali wakiwemo Maafisa Kilimo na Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia aliwataka kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya fursa zilizopo, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, ameagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha maafisa hao wanapatiwa mafuta wanapokwenda kazini badala ya kutumia fedha zao binafsi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Bwai Biseko, aliishukuru wizara kwa kuendelea kusaidia serikali za mitaa kwa nyenzo zinazorahisisha utendaji kazi.
“Tunaishukuru wizara kwa msaada huu mkubwa. Hii ni ishara kwamba serikali inatambua changamoto tulizonazo. Ni wajibu wetu kuhakikisha nyenzo hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Biseko.
Baadhi ya maafisa maendeleo ya jamii akiwemo Onesmo Msagati na Raphael Leonard kutoka Kata ya Bugandika walipongeza hatua hiyo na kuahidi kuzitumia pikipiki hizo ipasavyo ili kuchochea maendeleo kwa wananchi wa maeneo yao.










