Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya kuhitimisha kikao kazi cha siku mbili cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Kibaha Mkoani Pwani.
Mwenyekiti na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam (Brendan Maro na Sara Rwezaula-Kulia) wakimpokea Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipowasili Kibaha, Pwani kwa ajili ya kufunga kikao kazi cha Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la OSHA, Bi. Beatrice Lengereri.
Mkufunzi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada kuhusiana na masuala ya usalama na afya kazini katika kikao kazi cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi katika kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti na makatibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kuhitimisha kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Na Fredy Mgunda.
Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa Mkoa wa Dar es Salaam wapatao 180 wamepatiwa mafunzo ya awali ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwawezesha kuzishauri menejementi za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi na hivyo kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Mafunzo hayo yaliyowahusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote 90 ya TUGHE ya Mkoa wa Dar es Salaam, yamefanyika katika kikao kazi cha siku mbili Kibaha Mkoani Pwani ambapo viongozi wapatao 180 wameshiriki.
Pamoja na masuala mengine, mada mbalimbali zinazolenga kujenga uelewa wa jumla kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi zimewasilishwa na wataalam wa OSHA. Mada hizo ni pamoja na; Dhana ya Usalama na Afya mahali pa kazi, Uwakilishi na Kamati za Afya na Usalama mahali pa kazi, Mifumo ya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.
Wawasilishaji wa mada kutoka OSHA, Bw. Simon Lwaho na Moteswa Meda wamesisitiza washiriki kuwahamasisha wafanyakazi wenzao katika sehemu za kazi kujifunza kanuni bora za usalama na afya kutegemeana na shughuli zao za kila siku ili kupata mbinu za kujilinda dhidi ya vihatarishi mbalimbali vya magonjwa na ajali mahali pa kazi.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao kazi cha viongozi hao, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, aliyekuwa Mgeni Rasmi wa hafla ya kufunga kikao kazi hicho, amesema viongozi hao wanayo nafasi muhimu katika kushawaishi menejimenti za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi ili kuleta ustawi wa wafanyakazi.
“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza wenzetu wa TUGHE jitihada za serikali katika kuimarisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi ambapo mbali na kuiwezesha OSHA kusimamia uzingatiaji wa taratibu za usalama na afya, masuala haya yamejumuishwa katika kanuni za kudumu za utumishi wa umma. Aidha, uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya unaangaliwa katika ukaguzi wa CAG pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA nchini, Bi. Mwenda, ameahidi kuendelea kushirikiana na TUGHE pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi nchini wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na kanuni bora za usalama na afya zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao ya msingi katika hali ya ya usalama na kubakia na afya njema.
Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Komredi Brendan Maro ameielezea OSHA kama mdau muhimu katika utekelezaji majukumu ya chama chao.
“Tunawashukuru sana OSHA kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu hususan suala la kutoa elimu kwa wanachama wetu ambao ni wafanyakazi,” amesema Komredi Maro.
Akitoa neno la shukrani, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Norbetha Sanga ambaye ni Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) amesema mafunzo ya usalama na afya ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri ili kuwa na uzalishaji wenye tija.











