Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Sendiga, amezindua uchimbaji wa visima virefu 40 vya umwagiliaji, katika vijiji 40 vya Wilaya tano za mkoa, kwa lengo la kufikia malengo ya agenda 10/30 na visima hivyo vitaenda kuwanufaisha wananchi Zaidi ya 650 kwa awamu ya kwanza na kuongeza usalama wa chakula na kuleta kilimo chenye tija ndani ya mkoa.
Aliyasema hayo wakati akizindua mradi huo wa uchimbaji wa visima virefu 40 vya umwagiliaji, vya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NRC), katika kijiji cha Genda kuu wilayani Babati, Oktoba 23, 2025.
Aidha amewataka Wakurugenzi na mhandisi wa Tume, Richard Mgaya, wahakikishe kwamba wanasimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo, ambao Serikali imeweka fedha nyingi hapo.Na kusema kuwa kama Mkoa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2025/26 kuna zaidi ya bilioni 85 ambayo imewekwa kwenye masuala ya umwagiliaji.Na wakizisimamia vizuri hakika wataiona tija yake.
“Maelekezo yangu, ni ushiriki wa wananchi wenyewe kwenye maeneo yao, pamoja na viongozi wa vijiji ili kuweza kupata tija ya mradi huu.Ni muhimu hawa wataalamu ambao wapo sahizi huku wanaotafuta maeneo kwa ajili ya kuchimba visima, washirikiane na viongozi wa vijiji na wananchi wa kwenye maeneo hayo ili kusikiliza wenyewe wanasemaje kulingana na maeneo yao.” Alisema Mhe. Sendiga.
Sambamba na hayo alisema kuwa mitambo mitano ya uchimbaji wa visima, itaanza kufanya kazi katika Mkoa, na mitambo hiyo itafanya kazi kwa siku thelathini (30) zilizopangwa,na kwa awamu ya kwanza itachimba visima 40.
Pia amewataka wananchi waongeze ushiriki wao na ushirikiano mkubwa na wataalamu ambao wapo hapa mkoani, lakini pia wailinde miundombinu ya mradi huo na vifaa mbalimbali na kutoa wito wachangamkie fursa ya kilimo lakini pia wakulima wote wajisajili kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili wafanye shughuli zao kwa kufuata miongozo ya Serikali.
Mwisho ametoa rai kwa wananchi wa Gendi, ifikapo tarehe 29, Oktoba, 2025 washiriki uchaguzi mkuu na kwenda kuwachagua viongozi watakaokwenda kuwatumikia kwa miaka mitano, viongozi ambao watatanguliza mbele maslahi ya watanzania na wana Manyara kwa ujumla.








