Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amezipongeza kampuni mbili za Franone mining LTD na Chusa mining LTD kwa kusaidia miradi ya maendeleo katika utekelezaji wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwenye sekta ya afya mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
RC Sendiga akizungumza na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani, amesema makampuni hayo yanajitoa katika kufanikisha miradi ya maendeleo kupitia utekelezaji wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Ameeleza kwamba kampuni ya Franone mining LTD, imefanya vyema kwani imetenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ndani ya ukuta unazunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
“Pia niishukuru kampuni ya Chusa mining LTD, kwa kujenga wodi ya wanawake na watoto na ofisi ya wauguzi katika kituo cha afya Mirerani,” amesema RC Sendiga.
Hata hivyo, RC Sendiga amewataka wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo kupitia utekelezaji wa uwajibikaji kwa kijamii (CSR) kama ilivyo takwa la kisheria.
Ameeleza kwamba japokuwa wachimbaji wengi wamechangia CSR ila kasi kubwa inatakiwa kuendelezwa kwani mwamko siyo mkubwa katika eneo hilo la machimbo ya Tanzanite.
Mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Franone mining LTD, Francis Matunda ameeleza kwamba ujenzi wa zahanati hiyo katika machimbo ya madini ya Tanzanite itaanza kujengwa Novemba mosi mwaka 2025.
“Baadhi ya vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo vimeshafikishwa eneo la ujenzi na kazi ya kujenga itaanza mwanzoni mwa mwezi ujao,” amesema Matunda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa mining LTD, Joseph Mwakipesile Chusa, amesema ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto na ofisi ya madaktari katika kituo cha afya Mirerani inaendelea vyema.
Mwakipesile ameeleza kwamba ujenzi huo wa wodi ya wanawake, watoto na ofisi ya madaktari, unaotarajia kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2025 na kukabidhi kwa Serikali.







