Na Mwandishi Wetu- Geneva
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva na Mashirika Mengine ya Kimataifa, Mhe. Dkt. Abdallah Saleh Possi, aliongoza ujumbe wa Tanzania na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Huduma lililofanyika Oktoba 23,2025 wakati wa kikao cha kumi na sita cha Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD XVI) huko Geneva.
Jukwaa hilo lilijadili mikakati ya kutumia sekta ya huduma kuchochea mageuzi ya kiuchumi, utofauti wa uchumi na ukuaji jumuishi katika nchi zinazoendelea.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mhe. Dkt. Possi alisema kuwa sekta ya huduma ni mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ikichangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa, ajira na mapato ya mauzo ya nje. Amebainisha kuwa huduma za mawasiliano, fedha, usafirishaji na teknolojia zimeendelea kuimarisha sekta za uzalishaji kama kilimo, viwanda na utalii.
Aidha, Dkt. Possi alibainisha kuwa Tanzania, kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 na Sera ya Biashara ya Taifa ya mwaka 2023, imeweka kipaumbele katika kuimarisha biashara ya huduma ili kuongeza ushindani, kukuza mabadiliko ya kidijitali na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).








