Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa
WAKILI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa amesema kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni anakwenda kufungua kesi ya Kikatiba kuomba Mahakama itoe tamko kwamba kulipa tozo la Daraja la Kigamboni ni kinyume cha Katiba.
Wakili Majaliwa amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusiana na mchakato wa kufungua shauri la Kikatiba Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Amesema wamefikia hatua hiyo, baada ya kutumia mbinu mbalimbali ya kumaliza tatizo hilo lakini imeshindikana, wameamua kwenda kisheria zaidi ili kuondoa changamoto hiyo.
“Tunakwenda kufungua kesi kwa kuomba Mahakama itoe tamko tu kwamba kitendo cha wananchi wa Kigamboni au mwananchi yeyote kutoka nje ya Kigamboni kutaka kuvuka kuingia kulazimika kulipa tozo ya daraja ni kinyume na Katiba,”
“Na hasa kuzingatia juzi wastani wa mwezi mmoja umepita nilikuwa nimefuatilia uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya miaka 25 mbele sijaona nafuu kwa watu wa Kigamboni kuondosha tozo zile, “Amesema Wakili Majaliwa
Amesema utaratibu unaoendelea wa tozo hizo, unakizana na sheria zenyewe, sheria ambazo zinatumika kutoza tozo zipo za aina mbili, The Road Tolls (Fees) Regulations, 1985 (Kanuni ya tozo za barabara) na The Road and Fuel Tolls Act (Sheria ya tozo za barabara na mafuta).
“Ukizisoma sheria hizi mbili kwa pamoja kwa ujumla wake, mimi mwananchi wa Kigamboni nikitumia daraja kwa kuvuka kwa daladala au gari yangu binafsi naangukia katika kulipa kodi mara mbili,”amesema








